Serikali ya Tanzania imepanga kuweka uwekezaji mkubwa katika mkoa wa Mwanza kwa kutambua umuhimu wa mkoa huo katika kuchangia pato la taifa na kutokana na uwingi wa watu.

Kupitia kwa Msemaji Mkuu wa serikali Gerson Msigwa katika taarifa yake ya serikali ya wiki akiwa mkoani Mwanza, amesema Serikali inawapongeza wananchi wa Mwanza katika kazi za ujenzi wa taifa ikiwa ni pamoja na kuongeza pato la taifa kwa nafasi kubwa.

Msigwa amesema katika kipindi cha miezi sita ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mkoa wa Mwanza umepokea kiasi cha sh Billion 344 kwa ajili ya kuchangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo Jijini Mwanza ikiwa ni pamoja na kupanua kituo cha mabasi cha Nyamhongolo na Nyegezi, Soko la kisasa katikati ya jiji la Mwanza, jengo la abiria uwanja wa ndege na ujenzi wa meli kubwa ya MV Mwanza na Daraja la Kigongo Busisi.

Katika Sekta ya Afya serikali imetoa shilingi bilioni 15.2 kwa ajili ya hospitali za wilaya ya Sengerema, Misungwi, Kwimba, Buchosa na Ilemela ikiwa ni pamoja na vituo vya afya 5 na zahanatai 21 pamoja na kukarabati vituo vya huduma za jamii 48 bila kusahau Bilioni 6.4 kwa ajili ya kununua dawa.

Katika Sekta ya Elimu serikali imetoa shilingi Bilioni 38.7 kwa ajili ya miundombinu ya shule za msingi na elimu bila malipo, na kwenye mpango wa maendeleo ya jamii wa IMF mkoa wa Mwanza unatarajiwa kujengewa madarasa 985.

Katika Miundombinu ya Usafiri Mwanza imeendelea kupokea Mabilioni ya fedha katika kusimamia wakala wa barabara TARURA, REA na Miradi ya Maji na TASAF.

“Serikali imeendelea na dhamira yake ya kuliimarisha jiji la mwanza na tunataka Mwanza iwe kituo kikubwa cha kibiashara katika ukanda wa Maziwa makuu na jiji la kiuchumi kwa nchi yetu” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa Serikali pia inataka Mwanza iwe jiji la utalii ambapo wanatarajia kujenga Hotel itakayokua inaelea Majini katika ziwa Viktoria na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amefanya mazungumzo na wawekezaji ambao watachangia katika ujenzi huo.

“Halmshauri ya Jiji la Mwanza inaendelea na mipango yake ya kujenga Bustani ambayo itakua kivutio kwa watalii na sehemu za biashara na kupumzika ikiwa ni katika mahusiano mazuri na Mji wa Tempere wa Ujerumani.” amesema Msigwa.

Takwimu za sensa ya watu na makazi zinasema mkoa wa Mwanza ni mkoa wa pili kwa idadi kubwa ya watu ambao ni zaidi ya milioni tatu laki tisa ikiwa ni mkoa unaoendelea kuchangia vizuri pato la taifa ambapo mwaka 2020 imeshika nafasi ya pili kwa kuchangia shilingi trilioni 10.9.

Wananchi Sudan wapinga Serikali ya mpito
Masau Bwire aitakia ushindi Simba SC