Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) imetangaza mpango wa kumfikisha mahakamani Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (Udart), David Mgwasa kwa kile ilichoeleza kutoza nauli kubwa zaidi ya iliyokubaliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Mgewe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa abiria wakidai kutozwa nauli kubwa kuliko iliyoelekezwa awali, walifanya uchunguzi na kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo.

Mgewe alisema kuwa wamebaini kuwa ingawa inapaswa abiria anaetoka Mbezi Luis kulipia shilingi 400 hadi kimara na kulipa shilingi 400 nyingine anapofika Kimara na kutaka kuendelea na safari yake, Udart imekuwa ikimtoza abiria huyo jumla ya shilingi 1,050 (sh 400+sh650) badala ya jumla ya shilingi 800.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra alisema kuwa wamepanga pia kuwafikisha mahakamani madereva wa Mabasi ya mwendokasi wanaoendesha magari hayo kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 90 kwa saa badala ya kuwalipisha faini kama ilivyo hivi sasa.

Akijibu kuhusu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, Mgwasa alisema kuwa haogopi kupelekwa mahakamani kwa kile alichodai haiwezekani mtu alipe nauli hiyohiyo kwa safasi zake mbili tofauti.

“Haiwezekani mtu atoke Mbezi ashuke Kimara afanye shughuli zake halafu apande tena gari kwa bei ileile . Mimi siogopi, kama anapeleka mahakamani apeleke,” alisema Mgwasa.

Mgwasa aliomba kupelekewa ushahidi wa tiketi unaothibitisha kuwepo kwa ulipishwaji wa nauli kinyume na bei elekezi.

Zimebaki Saa 24 Kwa Gonzalo Higuain
Bordeuax Waridhishwa Na Kiwango Cha Mathieu Debuchy