Mwenge wa Uhuru umepokelewa mkoani Simiyu  ukitokea mkoa wa Shinyanga na kuanza mbio zake ,  mkoa ambao kwa mujibu wa ratiba ni mwenyeji wa kilele chake kitaifa tarehe 14 Oktoba  mwaka 2016

Akitoa taarifa ya mkoa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 , George Mbijima Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka , amesema Mkoa huo unatekeleza kwa vitendo Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 inayosema “Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na kuwezeshwa’’ kwa kuwawezesha vijana wote kutekeleza miradi ya maendeleo  kupitia kauli mbiu ya Mkoa wa Simiyu ya “Wilaya moja Bidhaa moja”.

Mtaka amesema Mkoa umewahamasisha vijana kujiunga katika vikundi na kuwapatia mitaji katika kutekeleza agizo la  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuwa nchi ya Viwanda.

“Utekelezaji umeanza na Mkoa wa Simiyu tumejichagua kuwa mkoa wa utekelezaji, Utekelezaji huo upo ambapo Wilaya ya Maswa ‘kwenye wilaya moja bidhaa moja’ inazalisha chaki na Meatu inazalisha maziwa”, alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema kiwanda cha kuzalisha chaki cha Wilaya ya Maswa kitafunguliwa rasmi na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Vijana, Ajira,Kazi na Wenye ulemavu,  Jenista Mhagama (Mb), tarehe 10/10/2016  ambapo pia tarehe 11/10/2016 atafungua Kiwanda cha kusindika maziwa Meatu.

Aidha kuhusu ujumbe wa kudumu wa Mbio za Mwenge  Serikali Mkoani Simiyu kwa kushirikiana na wadau wengine katika kupambana na madawa ya kulevya chini ya kaulimbiu ya “Tujenge jamii maisha na utu wetu;bila dawa za kulevya”  imeendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kwa wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Katika Mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kauli mbiu “Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI; Inawezekana” Mtaka  amesema mkoa unaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kupima kwa hiari virusi vya Ukimwi ili waweze kutambua hali zao na kujilinda na maambukizi mapya, kuachana na unyanyapaa na kuzuia vifo.

Hata hivyo kuhusu mapambano dhidi rushwa chini ya kauli mbiu “Timiza wajibu wako; kata mnyororo wa rushwa” Mtaka amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa inaendelea kuwachukulia hatua wote wanaobainika kutoa na kupokea rushwa  na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuelimisha kupitia klabu za wapinga rushwa mashuleni.                

Anthony Mtaka amesema Mwenge wa Uhuru  ukiwa mkoani humo utapita katika Halmashauri sita (6) ukianzia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Meatu, Itilima, Busega, Bariadi na Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuona miradi minne (4),  kufungua miradi tisa (9), kuweka jiwe la msingi miradi sita(06) na kuzindua miradi 11 ya maendeleo katika sekta ya Afya, elimu, maji, kilimo, barabara, sekta binafsi na utawala bora ambayo kwa ujumla wake ina thamani ya zaidi ya bilioni 12. 

NEC kuboresha Daftari la Wapiga Kura
Madereva wa Magari Yabebayo Mchanga Mkoa wa pwani Wailalamikia Tanroads