Shirikisho la Soka nchini TFF limesema msimu ujao litatangaza tenda kwa mikoa itakayokuwa tayari kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho (ASFC), na itapaswa kutuma maombi.

TFF imetoa kauli hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Ahmed Msafiri Mgoyi baada ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu 2019/20, kufanyika mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kwa mafanikio makubwa.

Mgoi amesema TFF itatangaza tenda sambamba na vigezo watakavyoviweka ili kupata mwenyeji wa mchezo wa fainali mwenye hadhi ya kitaifa.

Amesema mchezo wa Fainali wa mwaka huu ulioshirikisha klabu ya Simba SC ya Dar es salaam dhidi ya Namungo FC ya Lindi, zilikuwa bora zaidi kwa sababu ya kufanyia kazi changamoto zilizotokea katika Fainali zilizopita.

“Naamini mafanikio na shangwe zilizoonekana Sumbawanga katika fainali hii, itawaacha wadau wakiwa na mawazo chanya, tutaendelea kupeleka mashindano hayo katika sehemu mbalimbali hapa nchini, lakini fainali zijazo tutatangaza tenda kwa wanaohitaji kuandaa kuomba,” amesema Mgoyi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Rais wa zamani wa TFF na CECAFA, Leodegar Tenga, amesema amefurahishwa na uamuzi wa kupeleka fainali za Kombe la Shirikisho (ASFC) katika mikoa ambayo haina timu za Ligi Kuu na anaamini itachangia kuamsha hamasa mpya kwa wenyeji.

“Soka linaleta fursa nyingi, nimefurahishwa sana na fainali ya mwaka huu, hakuna kisichowezekana kama maandalizi yatafanyika, mechi kubwa kama hii huacha kumbukumbu isiyofutika, itaamsha na kuianzisha safari mpya Rukwa itafunguka sasa,” amesema Tenga.

Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema wataendelea kupeleka michezo hiyo na mingine mikoani ikiwa ni pamoja na ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21 (Ngao ya Jamii) kuchezwa Agosti 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Simba ambayo waliifunga Namungo FC mabao mawili kwa moja katika mchezo huo wa fainali ya ASFC iliyopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, timu hizo zitakutana tena katika kinyang’anyiro cha Ngao ya Jamii jijini Arusha.

Matola afichua siri ya kutwaa ASFC
JKT: wanafunzi kidato cha sita warudishwa kutokana na ujauzito