Mwenyekiti wa Majaji Wastaafu, Jaji Thomas Mihayo amepinga kauli za baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaodai kuwa Rais John Magufuli ni dikteta na ameingilia uhuru wa Mahakama.

Mwenyekiti wa Majaji Wastaafu, Jaji Thomas Mihayo

Mwenyekiti wa Majaji Wastaafu, Jaji Thomas Mihayo

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Mihayo ambaye alieleza kuwa amepewa baraka zote na Jaji Mkuu, Othman Chande kuzungumzia suala hilo baada ya kuona limezua mijadala mingi, Jaji Mihayo alisema kuwa wanaotoa madai hayo hawajui maana ya dikteta.

“Wanaosema Magufuli ni dikteta hawawajui madikteta. Hakuna kiongozi dikteta Afrika Mashariki isipokuwa Idi Amini tu,” alisema.

Jaji Mihayo alionesha kushangazwa na kauli za watu hao ili hali nchi nyingi za Afrika zinatamani Rais Magufuli angekuwa kiongozi wao angalau kwa muda wa miezi miwili tu, kutokana na kazi nzuri aliyoifanya ndani ya muda mfupi.

Akizungumzia madai ya baadhi ya watu kuwa Rais Magufuli aliingilia uhuru wa Mahakama kupitia hotuba yake aliyoitoa katika kilele cha siku ya mahakama, pamoja na ahadi yake kwa Jaji Mkuu kumpatia shilingi bilioni 12.3, huku akiahidi kuipa kada hiyo ya Mahakama shilingi bilioni 250 baada ya kushughulikia kesi za ukwepaji wa kodi zenye thamani ya shilingi trilioni 1, Jaji Mihayo alisema kauli hiyo haiwezi kuingilia uhuru wa mahakama.

“Uhuru wa mahakama upo ‘guaranteed (umehakikishwa)’ na katika kifungu namba 107 (a) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.Hata kama Rais akiamrisha vipi, kama ni kitu ambacho ni kinyume na utaratibu, hakiwezi kutekelezwa” Jaji Mihayo alifafanua.

Alisisitiza kuwa Rais Magufuli hajafanya jambo lolote ambalo linamfanya awe juu ya sheria, “Sijawahi kusikia kasema mfunge huyu au kusema sheria hii isitumike na hii itumike.”

 

Makamu wa Rais akanusha kuanzisha Vicoba, Saccos
Mhifadhi wa hifadhi ya taifa ya Ngorongoro ahusishwa utunguaji helkopita