Mtangazaji wa kipindi cha Leo tena kinachoruka kupitia Clouds fm, Mwemba Burton maarufu Mwijaku ameibua gumzo kote mitandaoni baada ya kujitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania, mapema leo januari 14, 2022.

Kinyume na fikra za wengi Mwijaku ameongozana na msafara wake maalum, mpaka Lumbumba jijini Dar es salam zilipo ofisi za Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya kuchukua fomu hiyo ya kuingia kwenye orodha ya wagombea wa kiti kilichoachwa wazi na aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai aliyejiuzulu Januari 6, mwaka 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwijaku ameyaweka wazi mambo kadhaa yaliyomsukuma kuamua kuingia katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo, licha ya watu kumfahamu zaidi kama mtangazaji, muigizaji na mhamasishaji wa mtandaoni.

“Nawashukuru baadhi ya viongozi, nimekuwa nikipata ushawishi mkubwa, wengi wamekuwa wakinipigia simu wakinihamasisha¬† wakiniambia kwamba Mwijaku tunakuhitaji uje utusimamie tuweze kulipeleka gurudumu la maendeleo mbele lakini mbali na hapo watanzania wamekuwa wakinitafuta kwa njia mbali mbali wananiambia Mwijaku umesoma na una elimu ambayo inatutosha kwa sisi watanzania kwenda kusimamia muhimili wa Bunge.” alisema Mwijaku.

Ameweka bayana namna alivyoguswa na kauli ya Rais wa Jamuhiri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusu heshima baina ya watu na nafasi zao.

Akitilia mkazo kwa kusema kuwa msukumo wa yeye kugombea nafasi hiyo umechagizwa na mchango wa serikali katika kumsomesha mpaka kufikia hatua hii.

“Kama nilisoma kwa kodi za Watanzania, mimi nisijivunie nikasimama nikasema kwamba nilisoma kwa pesa zangu, nitakuwa nimeongea uongo. Mimi nimesoma na kodi za Watanzania, nimepewa Boom na Serikali. Nimelipiwa Ada na Serikali.

Na huu ni wakati wa kurudisha fadhila zangu kwa taifa hili. Ndio maana nimeamua kuomba nafasi ya Spika, nimejiangalia viatu vinanitosha, elimu ninayo, ufahamu ninao na exposure ninayo. Niko tayari kwenda kumsaidia mama. Aliongeza.

Hii si mara ya kwanza kwa Mwijaku kuthubutu kugombea nafasi ya uongozi Serikalini, ikumbukwe mwaka 2020 alijitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge wa jimbo la Kawe jijini Dar es salam.

Ambapo alishindwa kuendelea baada ya kukosa kura za kutosha wakati wa mchakato wa kura za maoni kutoka kwa wajumbe wa CCM.

Waziri Bashungwa atoa maagizo kwa maaafis wa elimu
Zaka: Kigonya alistahili kadi nyekundu