Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana  kilivunja rekodi yake kilipozindua kampeni zake katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam baada ya kuwakusanya maelfu ya wananchi waliojitokeza kuwasikiliza viongozi wa chama hicho na hasa mgombea urais, Dk. John Magufuli.

Katika uzinduzi huo ulihudhuriwa na rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na rais wa awamu ya awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete ambao wote walirusha makombora upande wa wapinzani wakimpigia debe Dk. Magufuli.

Mzee Mwinyi alitumia nafasi hiyo kuivuruga ngome ya Ukawa inayoundwa na vyama vinne vikuu vya upinzani ambavyo ni Chadema, CUF. NCCR-Mageuzi na NLD akidai kuwa ngome hiyo inaongozwa na wafuasi wengi waliotoka CCM hivyo ni CCM B.

“Iweje uchague CCM B wakati kuna CCM A? Kwa hiyo mimi ninawaomba wananchi muipigie kura CCM A muachane na CCM B,” alisema Mzee Mwinyi.

Rais Jakaya Kikwete, Katibu wa CCM, Abdullrahman Kinana na Katibu wa Itikikadi na Uenezi,  Nape Nnauye wakifuatilia hotuba

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Shein, Rais Jakaya Kikwete, Katibu wa CCM, Abdullrahman Kinana na Katibu wa Itikikadi na Uenezi, Nape Nnauye wakifuatilia hotuba

Kauli hii ya Mzee Mwinyi inaweza kuchukuliwa kama changamoto kubwa itakayoikabili Ukawa kwa kuwa inafanana na ile aliyoitoa Profesa Ibrahim Lipumba baada ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CUF. Alisema kuwa katika uchaguzi huu, wagombea wote ni wanachama wa CCM.

Katika hatua nyingine, rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa aliwaponda Ukawa na mgombea wao kwa kutumia lugha yenye ukakasi akiwaita ‘wapumbavu na Malofa’, kauli ambayo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa muda mfupi huku ikichukuliwa kama udhaifu uliojitokeza.

Hii inaenda kinyume na onyo lilitolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupiga marufuku lugha za matusi katika mchakato huo kwa mujibu wa sheria.

Hivyo, kauli za Mkapa zinaweza kuchukuliwa kama point mojawapo itakayotumiwa na uapande wa upinzani ambao mgombea wao, Edward Lowassa aliahidi kufanya kampeni za kistaarabu zisizo na lugha za matusi. “Tutaenda hoja kwa hoja,” alisema Lowassa.

Lowassa Afanya Ziara Ya Kupanda Daladala Dar
CCM Kugawa Mamilioni Kila Kijiji