Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amemuingiza rasmi kiungo wake mkabaji, Abdulaziz Makame kwenye kikosi chake cha kwanza atakachokitumia kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa Afrika.

Zahera alibainisha hilo, Septemba 14, 2019 baada ya kumalizika kwa mchezo wa mzunguuko ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Zahera amesema kuwa alishindwa kumtumia kiungo huyo kwenye michezo iliyopita kutokana na kutokuwa imara. Aliongeza kuwa  bado anaendelea kumtengeneza kiungo huyo, kwa kumpa michezo ya mfululizo ili arejee katika kiwango na kuwa bora zaidi ya alivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Zesco.

Kocha huyo aliongeza kuwa kinachomshawishi aendelee kumtumia kiungo huyo ni umbile kubwa alilonalo, pia aina yake ya uchezaji ya kugongana huku akitumia nguvu nyingi na akili.

“Kwenye mechi hii na Zesco katika dakika ya 70 nilipanga kumtoa Makame baada ya kumuona amechoka, lakini nilimbakisha baada ya kuona umuhimu wake wa kuokoa mipira ya juu ya kona, faulo,” alisema.

“Lakini sikupanga kumtumia kwa dakika zote 90 kutokana na kukosa ‘match fitness’, Makame hakukaa na timu muda mrefu tangu ajiunge na Yanga, muda mwingi amekuwa na timu ya taifa, Taifa Stars.  “Hivyo, hakupata mechi nyingi za kirafiki kama walivyokuwa wachezaji wenzake, hivi sasa ndiyo ninaanza kumjenga na malengo yangu ni kumuona akiwa bora katika kikosi changu cha kwanza,” alisema Zahera.

Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, bao la Yanga lilifungwa na Patrick Sibomana huku lile la Zesco likipachikwa na Thabani Kamusoko.

DED na DC waliokuwa na mgongano watumbuliwa
Tume ya Madini yaiwakia kampuni ya TANCOAL, yaidai 'mabilioni'