Katibu Mkuu wa wizara ya elimu, sayansi na teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali imeaandaa mwongozo wa Kitaifa wa utoaji wa programu za mafunzo endelevu ya Walimu kazini ambayo yataongeza ufanisi wa kazi na motisha kwa walimu.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini unaotarajia kumalizika Novemba 6, 2019.

Amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha elimu kumekuwepo na changamoto mbalimbali hivyo mwongozo huo utasaidia kuondoa vikwazo vinavyojitokeza.

“Changamoto zipo licha ya jitihada za serikali katika kuzitatua hivyo huu mwongozo utasaidia kupata ufumbuzi katika programu za mafunzo kazini kwa walimu ikiwemo kutokuwa na mwendelezo na kukosekana kwa mfumo wa uratibu wa uendeshaji wa mafunzo,” amebainisha Akwilapo.

Aidha katika hatua nyingine Dkt. Akwilapo amewataka wajumbe wa mkutano huo kushiriki kikamilifu ikiwepo kutoa maoni ili kuandaa miongozo ya utekelezaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini nchini kwa lengo la kupata uzoefu kutoka kwa wadau.

“Wizara ya Elimu imeona ni muhimu kupata uzoefu kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kuhusu namna programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini zinavyoendeshwa naamini ushiriki wenu utasaidia kubaini maeneo muhimu katika kuratibu kazi zilizobaki,” ameongeza Dkt Akwilapo.

Amesema Serikali imekuwa ikitekeleza jambo hilo kwa miaka mingi ikiwepo mpango wa Tanzania, UNESCO na UNICEF na programu ya kutegemeza elimu ya msingi kiwilaya (DBSPE) hivyo uwepo wa muongozo huo ni muendelezo wa juhudi hizo katika kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika kwa ufanisi.

Awali Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema nchi yoyote iliyo makini huwa na wazo la kuwa na muongozo kuhusu mafunzo endelevu ya walimu kazini kwani bila uzingatiaji hayana tija kwani ni vitu viwili vinavyoenda pamoja.

“Tumeamua kwa dhati kwamba baada ya mafunzo ya awali ya walimu watakapokwenda kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi huko wakute wabobezi ambao watawapokea na kuendeleza kuwapa utaalamu siku kwa siku ili waweze kukua na kuendelea kitaalamu,” Amesema Dkt. Mutahabwa

Kwa upande wake mshauri wa elimu wizara ya maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza (DFID), John Lusingu amesema uamuzi wa Serikali kuitisha kikao hicho ni jambo jema kwani wanapata nafasi ya kuchangia kuboresha badala ya kufanyia kazi mawazo mtu mmoja.

Mkutano huo wa wadau wa kushirikishana uzoefu wa uendeshaji wa programu za mafunzo endelevu ya walimu kazini unashirikisha wadau mbalimbali kutoka Idara ya maendeleo ya Kimataifa (DFID), watafiti wa elimu kutoka Marekani (RISE), EQUIP-T, Tusome Pamoja, TAMISEMI na wenyeji Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia sanaa na ufyndi.

Video: Kichere awatumia salamu 'mafisadi', Kilio upinzani
Taasisi 16 zachangia Bilioni 236 serikalini