Na Edward Lucas

Utamu wa tendo la ndoa umepewa upekee wa kutolinganishwa na chakula chochote duniani, lakini kumbukumbu ya tendo hilo hutofautiana sana kati ya mwanaume na mwanamke. Utanielewa ukiendelea…

Binafsi nakumbuka sana utani wa rafiki yangu tuliyemtania kwa jina la ‘Ngoswe’, ambaye aliwahi kutuambia, “Unajua ni rahisi sana mwanamke hata aliyezeeka kukumbuka alijisikiaje mara ya kwanza kufanya mapenzi akiwa na miaka 20 hivi. Lakini ni vigumu sana kwa mwanaume aliyefanya mapenzi mara kadhaa, kukumbuka vizuri utofauti aliousikia alipofanya tendo hilo kwa mara ya kwanza.”

Ngoswe alitumia maneno yenye ukakasi kunilazimisha kuelewa alichokuwa anazungumzia ili nifahamu kuhusu mahusiano ya mapenzi aliponiona nimezama katikati ya kina cha penzi la mrembo mmoja aliyeniendesha kama gari lililokata break kwenye mteremko.

Huyo jamaa alinambia kuwa kinachoshangaza, katika maisha ya uhusiano, utamfanyia mwanamke kila kitu unachotaka, lakini kumbuka kuwa kwa kiasi kikubwa kumbukumbu yake hufutika na kurejea upya kana kwamba mmeanza jana tu. Sikumuelewa hadi yaliponikuta na kujikuta nikishindwa kusikitika hata kidogo nilipoambiwa kuwa mpenzi wangu ameambukizwa virusi vya ukimwi.

Najua wengi watashtuka sana kwa neno hili hasa wakijiuliza inakuaje mtu afurahi wakati mwenzie yuko kwenye matatizo. Lakini kwa upande wangu ni ngumu sana kudanganya kwa nafsi yangu kuitangaza huzuni isiyokuwa moyoni mwangu.

Nakumbuka siku ile aliyonitamkia kwamba hanihitaji tena alisema hakuna marefu yasiyo na ncha na kwamba amekaa na kutafakari kwa kina na kuona mimi siendani naye na kwa maana hiyo nitafute msichana mwingine na kama siwezi basi niwe ‘padre’. Daaaah!!!! iliniuma sana.

Nilisoma ujumbe wake wa kunikataa nikiwa kazini, nafundisha wanafunzi darasani huku kiu kali ya maji ikiniunguza koo kutokana na uhaba wa maji katika kijiji nilichopangiwa. Na sio tu kwamba kulikuwa na uhaba wa maji, mimi pekee ndiye mwalimu niliyekuwa nachagua sana maji ya kunywa, ‘lazima yawe yamechemshwa’ hivyo kuyapata pia ilikuwa mtihani zaidi.

Nilipomaliza kuusoma ujumbe wake, kwakweli nilishindwa kuuhisi ulimi mdomoni kwangu…mate yalinikauka ghafla. Ilibidi kipindi kiishie palepale..!

simuu

‘Nimeamua kuishi peke yangu, I need to be alone. Naomba uniache, tafuta mwanamke mwingine, mwalimu mwenzako atakuwa hadhi yako nadhani..! Ukishindwa unaweza kuwa padre mzuri,” ilisomeka sehemu ya ujumbe wake.

Haya yanaweza kuonekana ni maneno ya kawaida sana…lakini yalitoka kwa mtu niliyeweza kuwa naye katika mahusiano kwa zaidi ya miaka sita (6) na nikatumia nguvu kubwa ya kiuchumi kumsaidia katika elimu yake ya Chuo Kikuu. Baada ya kuhitimu, hii ndo zawadi ya maneno aliyoniandalia kwa muda wote huo. Kumbe tulikuwa wawili, mimi nikacheza nikijua ndio kila kitu.

Mwanzoni nilidhani anatania. Lakini kwa jinsi alivyosisitiza nikaanza kujiuliza kuna jambo gani baya lililomtatiza juu yangu hadi amepata maneno makali hivyo!! Akili nyingine ilinituma labda kuna mtu kamjaza habari za uongo juu yangu…lakini katika tafakari na kudadisi nilikuta hakuna kitu kama hicho.

Hii ilikuwa ni miezi miwili tu tangu ahitimu masomo yake ya Chuo Kikuu na kwa mipangilio na makubaliano yetu ni kwamba baada ya kuhitimu tutafanya taratibu za kuishi pamoja katika ndoa. Sikujua nilikuwa naota ndoto,  alinacha kwenye dunia ya Abunuasi.

Hili jambo liliniuma sana na kuanza kujiuliza kipi kipya sana kimeongezeka kwake hadi kuhisi siendani naye!!! Ni kwanini kwa kipindi chote hicho asiniambie kwamba hatuendani ili nitafute huyo wa ‘saizi’ yangu? Hadi amesubiri…nimehudumia kwa jasho kubwa na kazi yangu mshahara kiduchu, amehitimu chuo ndio anasema hivi. It’s so painful!

Haya mambo niliwahi kuyasikia kwenye wimbo mmoja wa zamani sana. Nikajua ni utunzi tu. Mwisho yakanikuta mwenyewe.

Siku tatu baadae, ambayo pia ni siku ya tatu baada ya kumaliza mitihani yake alinambia hataki tena simu kutoka kwangu wala meseji na kama nitakuwa na ujumbe basi nimpatie rafiki yake aliyekuwa akiishi naye hosteli atamfikishia…nilipomuuliza sababu za maamuzi hayo alinijibu kwa ufupi, “ukija tutaongea”. Na siku aliyokuja baada ya hiyo miezi miwili aliyokuja nayo ndio hayo.

Siku ya tatu iliwadia, nilijipanga sana kumshawishi ausikie moyo wangu. Lakini alisisitiza tena kwamba hahitaji nimpigie simu wala kumtumia meseji kwa sababu hayuko tayari kuwa katika mahusiano na mtu yeyote…na kweli zilipita siku mbili nikiwa bize kumtafuta katika simu bila majibu.

Nilipoendelea sana, niligeuka kuwa usumbufu kwake.

“We mwanaume… kwanini tunasumbuana hivi?? Unanimalizia chaji, nikwambie kwa lugha gani? Hivi huna kazi za kufanya au ndugu wa kuwapigia simu?” alinambia kwa ukali sana.

“Naomba nikwambie ukweli tu ndugu yangu…mimi nina mtu mwingine ambaye amekwisha nitolea mahari, sasa tayari unajua kinachofuata, tusiharibiane please.”

Kufikia hapo moyo ulishituka mithili ya sahani nzuri za udongo zilizodondoka kwenye vigae imara. Nilitaka kupiga kelele kwa sauti kama aliyeona jinamizi, Duuu!!! Kweli nilikubali kutoka jasho na kuhema sana sio lazima uwe umekimbia au kubeba mzigo.

Kipindi nikiwa bado nimepigwa ganzi ya maneno hayo.. nilimsikia akiendelea kuongea na kusema “tafadhali!! usipige simu yangu ovyo utaniharibia ndoa yangu……mimi sasa nina mume tena mpole kama huamini basi muulize mtu yeyote wa karibu yangu atakwambia…so jiheshimu” kisha akakata simu.

Hadi kufikia hapo kwa wale waliowahi kukutana na hali hiyo naamini wanayatambua maumivu hayo…kwahiyo wanaweza kuyahisi maumivu niliyokuwa nayo kwa wakati huo. Kiufupi tu ni kwamba inauma zaidi ya sana.

Machozi yalianza kunitiririka. Nilikunja sura na kulia kama mtoto aliyefinywa. Nikijiuliza, muda wote nimepigwa na vumbi la chaki, nimeamka asubuhi na mapema, nimejinyima kwa kila namna ili niweze kutimiza ndoto za mpenzi wangu katika elimu yake lakini hatua ya mwisho ananiambia tayari yeye ni mchumba wa mtu na tayari mahari kishatolewa!! Kwahiyo nilimsomeshea mwanaume mwingine!

Nilijiuliza kama amepata mchumba hata wa kufikia kumtolea mahari basi mahusiano yao yalianza kitambo kidogo. Sasa kwanini muda wote alikuwa akiomba pesa kutoka kwangu?? Hata hatua ya mwisho aliomba nauli kutoka kwangu akamalizie mitihani yake, kwanini asingemuomba huyo mchumba wake?

Basi… zilipita kama siku tatu pasipo kumtafuta huku nikiwa katika wimbi kubwa la mawazo hatimaye nilishindwa kujiuzuia na kuamua kumpigia simu….lakini maneno yaliyotoka hapo hadi nilijuta kupiga simu.

Baada ya simu kuita mara kadhaa bila majibu hatimaye alipokea na kusema kwa lugha ya ukali sana “hivi wewe!! unataka kunambia hata mama yako alishafariki umeshindwa kumpigia simu umekaa kunisumbua mimi? aliweka pozi kidogo kisha akaendelea

“Hivi vyalimu navyo sijui vipi……havielewi! Sijui huko darasani vinafundisha nini, We si nimekwambia sitaki unipigie simu wala kunitumia meseji au hadi nibadili hii namba kwa ajili yako ndio ujue namaanisha ninachokisema!? Alimaliza kwa kunisonya kisha akakata simu.

Daaaa!!!! kufikia hapo nilijihisi kama vile pakiti ya chumvi imesiginwa kwenye kidonda kibichi tena bila huruma.

Nikijiuliza huo ualimu wangu ulivyofanya kazi kubwa kumlipia ada na mahitaji mengine ya shule na awapo nyumbani..leo hii ualimu kwake ni kama tusi na ni kazi ya kudharaulika, kweli waswahili walisema bora umfadhili mbuzi unaweza kuambulia hata mchuzi kuliko binadamu asiye na shukrani.

Mtu ambaye alitakiwa anishukuru sana kwa juhudi zangu kwamba licha ya kuwa napokea mshahara kidogo niliweza kujinyima kwa kila hali ili niweze kumuandaa kuwa mke bora wa familia yangu hata wakati mwingine nashindwa kuwahudumia ndugu na rafiki zangu hatimaye naambulia matusi na dharau…inauma sana!!!!

Hakika uchawi binadamu wengine hawazaliwi nao ila machungu na maumivu wanayosababishiwa na binadamu wenzao huwafanya kuingia katika uchawi na ushirikina ili kutafuta faraja katika nafsi zao.

Kumbe inaweza isiwe zoezi gumu kubeba silaha na kutafuta uhai wa mtu au kumdhuru mtu, hii ni kutokana na binadamu kuwazamisha wenzao katika dimbwi la matatizo na majuto na wao wakakosa uwezo na hekima za kupambanua  Ukuu na Utukufu wa Mwenyezi Mungu katika kuchagua njia sahihi.

Lakini katika yote ushindi wa maamuzi unaweza kupatikana katika kile unachoamini hasa kufanya maamuzi ambayo hutojuta baadae . Hivyo, nilipiga moyo konde nikaomba hekima ya Mungu itawale katika maamuzi yangu na inipitishe kando katika mbigiri za kisasi zilizotanda moyo wangu nisahau yote.

Nashukuru kwa mapenzi ya Mungu niliweza kusahau na kusamehe yote yaliyopita nikawa bize na shughuli zangu za kutafuta maisha. Yaani tangu siku ile sikuwahi kumpigia simu wala meseji wala kumuulizia kwa jambo lolote yaani yeye na maisha yake na mume wake mimi bize na mambo yangu

Lakini cha ajabu hivi karibuni takribani miezi miwili iliyopita alinipigia simu na hii ni baada ya zaidi ya mwaka mmoja kupita pasipo kuwasiliana naye. Niliitazama simu nikaona ni namba ngeni lakini nilipopokea tu nilimtambua mapema kwa sauti yake.

Ambapo baada ya salamu alijikita moja kwa moja kuulizia maisha yangu…kabla sijamjibu chochote nilimuuliza, “Mbona bize na simu? Vipi huogopi kupoteza ndoa yako? Au sasa umeshaizoea?”

“Aaaaa!!! kawaida tu,” alinijibu kwa unyonge kabla hajaanza kuleta habari nyingine.

Niliongea naye kwa dakika kadhaa kisha nikakata simu na kuendelea na ratiba zangu..lakini tangia hapo amekuwa na mazoea ya kutaka kuongea nami hadi inafikia wakati analalamika kwa baadhi ya ndugu na rafiki zangu. Ndipo nilipopata taarifa zake kwamba ni kwa muda mrefu sasa wametengana na huyo mume wake…jamaa alimkimbia.

broken heart

Kwamba jamaa aliyemuoa baadae iligundulika ana mtoto mwingine nje. Alizaa na msichana waliyekuwa naye kitambo. Eti baada ya miezi kadhaa jamaa akawa kaegemea zaidi kwa yule mwanamke mwenye mtoto wake. Mtoto alikuwa na nguvu kubwa. Ilifikia wakati jamaa akamtolea mahari kabisa yule dada na kuanza kuishi naye sehemu nyingine.

Kipindi naendelea kuyapata haya wiki iliyopita alinipigia simu na katika mazungumzo alianza kulaumu.

“Nyie wanaume ni mbwa kabisa….yaani mna maneno mazuri mkiwa mnamuhitaji msichana, mkishampata mnamuona takataka kabisa hafai”. Nilimuwekea kituo kidogo kwa kumuuliza, “hayo sasa yanakujaje!?

Alianza kunieleza maneno mengi na matukio ambayo amekutana nayo kwa huyo mume wake. Ilikuwa filamu mpya ya mateso. Kwa kweli ni mambo mazito sana yakutia huruma ukilinganisha na muda walioishi. Lakini kwa upande wangu nahisi moyo wa huruma ulishazikwa na mambo aliyokuwa amenifanyia. Hivyo, sikuguswa na mikasa hiyo.

Baada ya kumaliza kuongea nikiwa nimemsikiliza kwa makini, nilijikuta nashindwa kumuonea huruma. Shetani wa kisasi aliweka tabasamu kwenye sura yangu.

Nikajikuta namwambia, “Daaaa!! hayo ndo matendo ya mume mpole mwenye hadhi yako!? ‘Anyways’, nashindwa nikushauri nini kwa sababu hauendani  na ‘twalimu’ kama sisi. Hayo ya kizungu hatuyajui sana. Baadae basi.. kuna kazi nafanya tutasimuliana hizo filamu baadae,” nikamaliza na kukata simu.

Niliamini kwa maneno hayo yatamkumbusha vituko alivyonifanyia asidhani nimesahau sana…sambamba na kunitafuta kwa salamu za hapa na pale katika simu.

Ni kama alinisimulia mateso lakini alisahau suala moja kubwa lilokuwa linamkabili. Siku moja nilikutana na rafiki yake mmoja, mpambe wake wa karibu sana. Alinipa habari ya kusikitisha. Alieleza kuwa miezi kadhaa baada ya kuolewa alijikuta yeye na huyo mumewe ni waathirika, walipata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Kwamba suala hilo lilikuwa sehemu ya kichochezi iliendelea kuwa kichochezi cha wao kutengana.

Wakati dada yule ananisimulia kisa hicho kibaya na cha kusikitisha, nahisi yule shetani wa visasi alinirudia tena bila aibu. Nilijikuta naguna ‘kinafiki’, lakini tabasamu… mara ghafla kicheko kilichonibana kilitoka. Yule mpambe hakunielewa kabisa. Lakini tayari hilo lilikuwa limetokea.!

Yule dada aliniuliza, “unacheka nini?” nikawa sina cha kujibu, nilijisikia nimeupenda ghafla Ukimwi ulio ndani ya yule mrembo niliyempenda na kuwekeza kwake. Shetani wa kisasi alinizidi nguvu na kuniabisha mbele ya yule rafiki yake.

“Hivi wewe una ukichaa..!?  Unacheka kama vile umeshamaliza maisha hapa duniani! Wewe unadhani una guarantee ya kuishi milele.. unajua utaugua ugonjwa gani kesho?”

Yule dada alinisema sana hadi nikaanza kurudiwa na akili yangu ya awali. Alitaka kuondoka kwa hasira. Nikamuomba msamaha kwa kuwa nilitaka kusikia nini kilitokea tena lakini aliondoka kwa hasira huku akisonya.

Niligundua kitendo kile alichonifanyia, kiliniumiza kwa muda mrefu na kuniondolea ‘utu’. Nilijiona mshindi wakati huo, wakati yeye akiwa katika hali ya maumivu. Kwakweli nilipenda Ukimwi uliokuwa unaishi ndani yake.  Bila kujua nilikuwa nimeingiwa na shetani mbaya wa kisasi.

Miezi mitatu baadae, nilipata likizo. Ilikuwa mwezi Disemba, watoto walikuwa wamefunga shule. Nikaona bora nielekee jijini Dar es Salaam nikasafishe macho. Nilialikwa na rafiki yangu Joel. Fundi wa vifaa vya umeme anayefanya kazi na kampuni moja maarufu la vifaa vya umeme jijini hapo.

Siku moja, kama unavyoweza kuona kwenye filamu. Niliamua kutoka na kuzunguka Dar. Kama kawaida, Mlimani City ndo sehemu ya kwanza kwangu. Nikaangaze angaze tu.

Ghafla, nilimuona yule msichana akipita kuelekea mlango wa kutoka, mimi nikiwa ndani naelekea mbele. Kama tunapishana naye. Alinisalimia huku akitabasamu. Ila tabasamu lile lilikuwa la shida kidogo. “Mambo,” alisema kwa sauti ya kusita. “Poa…mambo,” niliitikia kama nimeshtukizwa.

Tulipishana, kila mmoja akashika njia yake!

Baada ya hatua nne niligeuka, nikakuta naye amegeuka kuniangalia na macho yetu yakagongana. Aligeuka kwa aibu na kuendelea.

Hali ya huruma iliiniingia. Nikazunguka lango la pili nikaongeza mwendo wa hatua zangu nikamuwahi pale nje. “Mambo vipi kwa mara nyingine,” nilimwambia. “Poa tu…” alinijibu huku akiangalia chini. Macho yake yalianza kuonesha unyevu, alikuwa anataka kutoa machozi.

Nilimpokea mizigo michache aliyokuwa amenunua, nikamuomba tukae kidogo kwenye moja ya mgahawa ulioko hapo nje ya Mlimani City.

Nilimwambia ninafahamu yote yaliyomkuta. Niliingiwa na hali ya utu ghafla. Wakati huu yule shetani wa kisasi hakuwa na mimi tena. Niliongea naye kwa upole. “Ulinikosea, nimekusamehe… Nilikukosea pia, nisamehe,” nilimwambia. “Naomba unisamehe p-please,” alianza kulia tena.

Niliingiwa na huruma kubwa, nikakumbuka niliwahi kuwa sehemu ya kampeni moja ya kuhusu Ukimwi, inaitwa ‘Ishi’ mwaka 2003/ 2004. Niliutumia uzoefu huo kuongea naye na kumshauri pia. Alionekana mnyonge, nilimuahidi nitakuwa rafiki yake wa karibu tena.

Alifurahi huku akitoa machozi wakati mwingine. Tulizungumza mengi. Akanipa namba yake mpya ya simu. “Naishi Sinza kwa Remmy na dada yangu,” alisema. Alikuwa anafanya kazi katika kampuni moja ya simu. Lakini kutokana na msongo mkubwa wa mawazo aliamua kuacha kazi apumzike nyumbani.

Nilimsihi sana atafute kazi na maisha yake yaendelee kwani kupata virusi vya ukimwi sio mwisho wa maisha. Maisha yanaendelea.

Alifurahi kusikia hayo kutoka kwangu, tulikuwa marafiki wapya na tulitembeleana tena. Tukafarijiana huku nikimtania, “nimekuwa padre tayari na wewe ushakuwa Sister.”

Utunzi wa Edward Lucas; 0655 545 064

 

 

Mwanasiasa apendekeza wakimbizi wapigwe risasi
Inasikitisha: Kijana aota 'mizizi' mikononi na Miguuni kwa kupata virusi hivi