Makamu mwenyekiti wa Young Africans Clementy Sanga ameombwa atangaze kujiuzulu kama ilivyokua kwa aliekua bosi wake Yusufu Manji.

Ombi hilo kwa Clement Sanga, limetolewa na katibu wa baraza la wazee wa Young Africans Ibrahim Akilimali, alipozungumza na Dar24.

Akilimali amesema Sanga anapaswa kujiuzulu, baada ya kushindwa kuiendesha klabu ya Young Africans tangu alipoondoka Yusufu Manji, hususan katika suala la usajili wa wachezaji ambalo limeanza rasmi hii leo kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF.

Mzee huyo alifikia hatua ya kumuomba makamu mwenyekiti akae pembeni, kutokana na tuhuma anazorushiwa na baadhi ya wanachama wenzake kwa kumwambia amekua chanzo cha matatizo yanayowasibu kwa sasa, kutokana na maneno yake ambayo yanaaminika kuwa chanzo cha kujiuzulu kwa Yusufu Manji.

“Naomba niwajibu baadhi ya wanachama wenzangu wanaojaribu kunitumia ujumbe katika simu yangu ya mkononi kuhusu suala la kuondoka kwa Yusufu Manji, na wengine wanadiriki kuniomba niende klabuni ili nifanye usajili wa wachezaji.

“Binafsi nipo tayari kufanya hivyo, lakini kwa sharti la kumtaka Sanga ajiuzulu, ili atoe nafasi kwangu ya kufanya kazi hiyo, nikifika klabuni kila mmoja ataona namna nitakavyofanya, maana hela za usajili zipo.

Kuhusu maamuzi ya kupinga Young Africans isikodishwe, Akilimali amesema alikua na haki ya kufanya hivyo kwa maslahi ya klabu hiyo, ambayo ni mali ya wanachama.

“Mimi pamoja na wenzangu hatukuwa na nia mbaya ya kupinga Young Africans isikodishwe, tulimaanisha klabu yetu haiwezi kumilikiwa na mtu mmoja halafu awe na mamlaka na kila kitu.

“Nilikua na wenzangu, na sote tunaamini Young Africans ni ya wanachama, sasa kama niliyoyasema yamewakera basi, lakini mimi nilimaanisha Young Africans inastahili kuendelea kuwa mikononi mwa wanachama.” Amesema Akilimali

Wakati huo huo Akilimali ameahidi kufika kwenye makao makuu ya klabu ya Young Africans mara baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kama ilivyokua siku za nyuma, ikiwa ni ishara ya kutomuhofia mtu yoyote klabuni hapo.

Phil Jones: Karibu Victor Lindelof
Kimenuka! Mayweather na McGregor, waweka wazi tarehe ya pambano

Comments

comments