Ni dhahiri kuwa tangu mzee Kingunge Ngombale Mwiru ajiunge rasmi na kambi ya Ukawa, kitu cha ziada kimeongezeka kwenye kambi hiyo ingawa sirasimishi kuwa kuna kitu kimepungua upande wa pili.

Mwanasiasa huyo mkongwe anaeaminika kuwa mmoja kati ya wachora ramani za ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, pamoja na kuwa mwenyekiti wa uandishi wa ilani zote za chama hicho kasoro ile ya awamu hii, hivi sasa amepewa rungu na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, na yuko kati ya wazungumzaji wakuu kwenye mikutano ya kampeni ya Lowassa.

Kama unasoma ‘katikati’ ya mistari, Mzee Kingunge hivi sasa hukaa karibu na Lowassa na huwa wanateta mara kadhaa (huenda anamchorea ramani).

Kwa waliomuona mzee Kingunge kwenye mikutano yote ya Lowassa, watakubalina na mimi kuwa mzee huyu anaonekana kuwa mwenye furaha kubwa, vijana wa kisasa wanaita ‘mzuka’ kila anapoona umati unaomsapoti Edward Lowassa. Hii inatokana na imani ya mzee huyo kuwa Lowassa anafaa kupewa ridhaa na wananchi kuongoza serikali ya awamu ya tano kama alivyokuwa akimtabiria tangu alipokuwa CCM.

Mzee Kingunge 'akimchorea' Lowassa ramani ..

Mzee Kingunge ‘akimchorea’ Lowassa ramani ..

Mzee Kingunge, juzi alitoa siri ya inayomfanya Lowassa kuwa na nguvu kubwa na kuufanya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa uchaguzi wa kihistoria dhidi ya chama chake cha zamani, CCM ‘kilichomkata kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni za kumpata mgombea urais.

Akizungumza katika jukwaa la kampeni la Lowassa jijini Mwanza, Mzee Kingunge alisema kuwa CCM ndio wanaompa Lowassa nguvu kubwa aliyonayo hivi sasa!!

Je, hiii ina maanisha kuwa CCM wanashiriki kunoa silaha dhidi yao wenyewe? Ndio maana nauliza, Ya kweli hayo?

Lakini ufafanuzi wa Mzee Kingunge unazidi kuniongeza tafakuri zaidi, pale alipoeleza kuwa CCM wanamuongezea nguvu Lowassa kutokana na jinsi wanavyomshambulia na kumtukana majukwaani, matusi hayo yanafanya wananchi wampende zaidi! Hapa nauliza tena, Ya kweli hayo?

Kama nimemuelewa vizuri mwanasiasa huyu mkongwe, nguvu ya kumshambulia adui yako kisiasa inapokuwa kubwa sana, unaweza kujikuta unamuongezea umaarufu zaidi kwa jinsi unavyomshambulia.

Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kisiasa nchini wamewahi kueleza kuwa jina la Edward Lowassa ndilo jina lililoongoza kwa kutamkwa zaidi katika majukwaa ya siasa, iwe kwa uzuri au ubaya. Katika mikutano ya CCM, jina la Lowassa limekuwa likitajwa mara nyingi zaidi kulinganisha na jinsi ambavyo jina la Magufuli linatajwa katika majukwaa ya wapinzani! Hususan hapo awali ambapo timu ya watu 32 ya kamati ya kampeni ya CCM ilipoanza kazi yake.

Huenda hicho ndicho kitu alichokizungumza mzee Kingunge Ngombale Mwiru, moja kati ya waliokuwa wachora ramani za ushindi za CCM aliyehamia kambi ya maadui. Je, uamuzi wake utazaa matunda? Au CCM itakizamisha chombo alichokimbilia?

CCM haipaswi kuyapuuzia maneno ya Kingunge bali iyachukue kama siri ya adui, waitafakari na kufanya maamuzi. Naamini hizi siku 11 zilizobaki ni sawa na siku za mgonjwa ambaye anaweza kutumia dawa yoyote kwa majaribio akitafuta kupona. Hali ni tete kwa pande zote… ni vigumu kumtabiri mshindi, lakini kitendawili hiki kitateguliwa kwa kuhesabu kura za watanzania Oktoba 25.

 

J Makamba Adai Magazeti ‘Hutumiwa’ Kuandika Ndivyo Sivyo Kuhusu Lowassa
CCM Wampania Lowassa, Watosa Kukutana Na Wagombea Wengine