Ikiwa ni mwaka mmoja tangu Dkt. John Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amempa sifa za utendaji uliotukuka.

Akizungumza leo muda mfupi baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam, Mzee Mwinyi alipongeza juhudi na kazi aliyoifanya kwa kipindi hiki kifupi, akidai kwa mtazamo wake amezidi kazi waliyofanya watangulizi wake.

“Sisi tuliopita, tulijitahidi kufanya kazi kwa kadiri ya uwezo wetu… lakini kazi aliyoifanya Rais Magufuli kwa mwaka mmoja tu naweza kusema inazidi kazi tuliyoifanya sisi,” alisema Mzee Mwinyi.

“Rais Magufuli amefanya vizuri kupitiliza,” alisisitiza na kufafanua kuwa pamoja na mambo mengine amerejesha nidhamu na uadilifu kwa watumishi wa umma.

Rais Magufuli amekuwa akisifiwa hata na mataifa ya nje kwa kazi aliyoifanya kwa kipindi hiki kifupi ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi.

Video: Rais Magufuli anafanya kazi nzuri sana - Mwinyi
Video: Waliozuia Mkutano wa Maalim Seif ni viongozi wa Mtwara, Alienda na ajenda mbovu - Prof. Lipumba