Mchungaji wa Kanisa la Maombezi lililoko Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako amesimulia jinsi alivyokumbana na kejeli ya askari polisi kuhusu sakata lake la kulewa na kumtolea matusi jirani yake.

Siku kadhaa zilizopita, Mzee Upako aliripotiwa kukamatwa na jeshi la polisi kufuatia mkasa wa kumtolea matusi jirani yake huku taarifa zikidai kuwa alibainika kuwa alikuwa amelewa pombe.

Akihubiri kanisani kwake Jumapili iliyopita, Mzee wa Upako alisimulia mkasa wake na afisa wa Jeshi la polisi alipokuwa katika makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Wiki iliyopita nilikuwa wizara ya mambo ya ndani, baadhi ya maofisa wakaniona, wewe mzee wa upako, wewe mzee wa upako, askari mmoja akaniuliza unachukua sadaka unaenda kunywa pombe. Nikawauliza hiyo pombe nilikunywa wapi, halafu pombe zipo nyingi, taja ni pombe gani, ukienda mbali zaidi ungeuliza nililewa nini, maana hata upako wa roho mtakatifu ni ulevi,” anakaririwa.

Licha ya awali kudai kutozungumza hadi mwezi mmoja upite, mhubiri huyo amekuwa akizungumza vipande vichache vya mkasa huo. Alikanusha tuhuma za kulewa pombe na kuwaonya waliosambaza habari hizo alizodai ni za uongo.

Utafiti Mpya: Pombe ni hatari kwa Moyo wako, fahamu kiasi usichopaswa kuvuka
Rais Magufuli, Dangote kuteta Ikulu baada ya kiwanda chake kuzima