Mchungaji wa Kanisa la Maombezi la GRC, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako amesema kuwa jina la waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa bado ni tishio kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na namna lilivyotajwa mara kadhaa katika mkutano mkuu maalum wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mzee wa Upako alisema kuwa Lowassa anaonekana kuwa mtu tishio katika chama hicho kutokana na uzoefu wa uchaguzi mkuu uliopita.

“Lowassa ni tishio, jina lake kutajwa sana kwenye mkutano wa CCM inaonesha kuwa ni mtu tishio,” alisema Mzee wa Upako. “Ilikuwa ngumu kukwepa kutaja jina lake katika mkutano huo maalum wa CCM,” aliongeza.

Lowassa

Aidha, alishauri vyama vya siasa kutumia muda huu kutibu majeraha ya mpasuko yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliopita na kukataa kuendeleza uhasama kati yao.

“Nasema hivyo kwa sababu naona hawa makada wanarudi kwenye vyama vyao kama CCM na Chadema wanaishia kupigana vijembe tu na kuendeleza majadiliano yasiyokuwa na msingi,” alisema Mchungaji huyo.

Jina la Lowassa lilitajwa mara kadhaa kwenye mkutano mkuu maalum wa CCM uliofanikisha kumkabidhi uenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Lowassa aliihama CCM mwaka jana na kujiunga na Chadema na kusababisha mtikisiko mkubwa katika chama hicho. Baadhi ya viongozi wa ngazi za mkoa na wilaya wa chama hicho walimfuata.

Paul Pogba Awachanganya Mashabiki Wa Man Utd
Video: Jambo Alilosisitiza Rais Magufuli Kwa Muda Wa Siku Tatu