Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson ameripotiwa kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kujietetea dhidi ya maombi yaliyowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya (Chadema) akimtaka aondolewe kwenye nafasi hiyo.

Katika maombi yake, Mallya anataka Bunge limuondoe Naibu Spika kwa kile alichoeleza kuwa anaendesha vikao kwa upendeleo, ukandamizaji na kuvunja kanuni hivyo hawana imani naye.

Kwamujibu wa taarifa zilizopatikana miongoni mwa wabunge, Naibu Spika tayari ameshahojiwa na Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, George Mkuchika.

Hata hivyo, Mkuchika aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawezi kuzungumzia kile kinachoendelea ndani ya Kamati hiyo kama Mwenyekiti.

“Siruhusiwi kusema nani kaitwa kwenye vyombo vya habari, Kamati yetu inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria,” alisema Mkuchika.

Naibu Spika anakuwa kiongozi wa Kwanza kwa cheo hicho kuhojiwa na Kamati hiyo kujitetea kuhusu ombi la kuondolewa katika kiti hicho. Baada ya kukamilika kwa taratibu za Kamati hiyo, endapo itaona inafaa, itawasilisha suala hilo Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Spika wa Bunge ndiye anayefaa kukalia kiti kuongoza mjadala wa hoja ya Kumng’oa Naibu Spika.

 

Mwigulu Nchemba atangaza Kiama cha ‘Wauza Unga’
Salute kwa Wabunge kufyeka mishahara ya Polisi