Na Allawi Kaboyo – Bukoba

Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika mji wa Kemondo mkoani Kagera.

Mradi wa maji wa Kemondo unatekelezwa kufuatia ahadi aliyoitoa Rais Dkt. John Magufuli wakati akiomba kura mwezi Oktoba mwaka 2020 kwa wananchi wa Kemondo.

Akizungumza na wananchi wa Kemondo wilayani Bukoba Machi Mosi mwaka huu katika ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amepongeza BUWASA pamoja na RUWASA kwa utekelezaji wa haraka wa mradi huo.

“Ni matumaini yangu kuona wananchi wa Kemondo wanapata huduma ya maji safi na salama mapema iwezekanavyo, hivyo tuna kila sababu ya kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huu kwa wakati,” amesisitiza Mhandisi Mahundi.

Mhandisi Mahundi ameagiza ufanyike utaratibu wa kuongeza nguvu kazi ili vifaa vilivyopo katika eneo la mradi viweze kufanyiwa kazi kwa haraka na ikiwezekana kazi zifanyike usiku na mchana ili mradi ukamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mahundi, mradi huo utakapokamilika utahudumia kata sita zenye vijiji 17 kwa awamu 3 ambapo awamu ya kwanza itakuwa kata ya Kemondo yenye vijiji viwili, ambapo litajengwa tenki la lita milioni 3, mtandao wa mabomba, (raising main) kwa gharama ya shilingi bilioni 6.8, huku wakiwa wameshapokea shilingi milioni 600.

Awamu ya pili itagharimu shilingi bilioni 7 na itahusisha Kata nne za Maruku, Kanyangereko, Bujugo na Katerero na awamu ya mwisho itahusisha Kata ya Muhutwe ambayo kazi zake zitagharimu shilingi bilioni 3.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mahundi amekagua mradi wa maji wa Kyaka Bunazi uliopo katika Wilaya ya Misenyi unaotekelezwa kufuatia agizo alilolitoa Rais Magufuli tarehe 11 Julai, 2019, ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 48 na utakapokamilika utahudumia wananchi wapatao 65,000.

Kaze azikasirikia Tanzania, Burundi
Othman Masoud aapa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar