Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaagiza watendaji wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatumia kwa wakati fedha wanazopokea kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.

Ameyasema hayo katika ziara ya kikazi wilayani Kisarawe baada ya kubaini kuwa zaidi ya shilingi milioni 100 hazijatumika katika kutekeleza mradi wa maji wa bwawa la maji la Chole wilayani hapo.

“Hili jambo tumeongea kwa muda mrefu kuwa fedha zinazoingia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zitumike kwa wakati Mvua zimeisha muda mrefu. Wewe bado una zaidi ya shilingi milioni 100 kwenye akaunti wakati wananchi hawajapata huduma ya majisafi na salama Hili halivumiliki,” Amesema Mhandisi Maryprisca.

Ameongeza kuwa serikali inatoa fedha kidogo kidogo kulingana na hatua ya utekelezaji wa miradi na haiwezi kupeleka fedha katika maeneo ambayo bado kuna fedha ambazo hazijafanyiwa kazi.

Aidha amewaasa wataalamu wa Wizara ya Maji kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA, wilaya ya Kisarawe Mhandisi Majid Mtili ameeleza kuwa RUWASA imejipanga kufikisha majisafi na salama vijijini ili kupunguza kero ya upungufu wa huduma ya majisafi na salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Saimon amesema serikali inatambua changamotro ya upatikanaji wa huduma ya maji katika wilaya hiyo na kwamba itahakikisha inatatuliwa.

Amesema kwa sasa kiwango cha upatikananji wa maji kwa vijiji vya wilaya ya Kisarawe ni asilimia 65 na kwamba mpango uliopo ni kuongeza huduma hiyo hadi kufikia malengo yaliyoainishwa ya asilimia 85.

Pro. Ndalichako azitaka taasisi za sayansi kufanya tafiti
Serikali yatoa tamko miamala kutolewa