Serikali imesema Vijana ni kundi tegemewa kwa Taifa kwani wanabeba dira ya Taifa kutokana na mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa hivyo wanapaswa kulindwa dhidi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo UKIMWI na vitendo vya ukatili.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu Wenye Ulemavu Ummy Nderiananga wakati akizindua Programu ya ONGEA Kitaifa Jijini Dodoma yenye lengo kuwafikia Vijana nchi nzima kupata uelewa wa masuala ya Maambukizi virusi vya UKIMWI kupitia vyombo vya habari.

Naibu Waziri Ummy ameeleza kuwa Uzinduzi wa programu ya kimataifa ya ONGEA ni fursa ya kuwafia vijana balehe nchini kupitia vyombo vya Habari ili kuwaongezea uelewa kuhusu matatizo na changamoto zinazowakabili katika Maisha yao ya kila siku ikiwemo maambukizi ya VVU ili wachukue hatua za kuandaa mikakati mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hizo.

“Serikali kupitia uongozi wa Mheshimwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan tunaamini vijana ndio waliobeba taifa letu na ndiyo nguvukazi ya nchi kwa hiyo kwa pamoja lazima lazima tuhakikishe ushirikiano unakuwepo katika kulinda afya zao,” amesema Naibu Waziri Ummy

Aidha, Ummy ametoa wito kwa Vijana nchini wafuatilie maudhui ya programu hiyo ya ONGEA kwa kina huku akifafanua kuwa programu hiyo itakuwa ya miezi tisa lengo likiwa kuwafikia Vijana zaidi ili waweze kuondoa vikwazo kwa Vijana balehe kupitia vipindi vya redio.

“Kupitia programu hii tufanikiwa kuongeza uelewa pamoja na ongezeko la upimaji wa afya kutoka asilimia 43 mpaka 57 hivyo kutakuwa na manufaa makubwa,”

Majaliwa:Nimeridhishwa na hatua ya ujenzi wa SGR
Rais Samia kupokea taarifa ya Soko la Kariakoo