Mhudumu wa hoteli ya kifahari ya Dusit D2 jijini Nairobi iliyoshambuliwa na magaidi wa Al-Shabaab Januari 16, amesimulia jinsi alivyowahudumia magaidi hao kahawa siku mbili kabla ya tukio hilo na kilichotokea baada ya kukutana nao kwenye tukio.

Mhudumu huyo ameeleza kuwa amewakumbuka magaidi hao kuwa ni wale aliowahudumia kahawa siku mbili zilizopita kama wateja, baada ya kumuona mmoja wao siku ya shambulizi akiwapiga risasi rafiki zake sita lakini akamuacha yeye na kumpa ujumbe.

Mhudumu huyo ambaye jina lake halikutajwa, amewaambia waandishi wa habari kuwa anamkumbuka mshambuliaji huyo kwakuwa alikuwa ana kovu kubwa mkononi.

Picha ya mmoja wa Magaidi iliyochukuliwa kwa CCTV Camera

“Nilimfahamu kwa kuwa nilikuwa nimemuona ana kovu kubwa kwenye mikono yake. Niliwaona tena wakiwapiga risasi rafiki zangu sita, wanne hawakufa palepale lakini wawili walipoteza maisha,” alisimulia.

Alisema kabla ya kumuacha aondoke, walimpa ujumbe wakihoji kwanini Wakenya wanawaua ndugu zao nchini Somalia.

“Kwanini mnawaua kaka na dada zetu Somalia? Hawahudhurii Madrassa tena,” anasema mmoja wa washambuliaji alisema kabla ya kufyatua tena risasi lakini hakumlenga yeye.

Watu 14 waliuawa katika shambulizi hilo kwa mujibu wa Serikali ya Kenya, na takribani watu 700 waliondolewa wakiwa salama kwenye jengo hilo.

Magaidi wote waliovamia jengo hilo waliuawa na hali ya usalama na utulivu ilirejea huku watu tisa wakikamatwa ikiwa ni pamoja na mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa alikuwa mke wa mshambuliaji mmoja.

LIVE: Rais Magufuli akikabidhiwa mfumo mpya wa kusimamia mawasiliano ya simu (TTMS)
Kilaba ataja faida za mfumo mpya wa mawasiliano

Comments

comments