Baada ya picha za CCTV kuonesha sura za magaidi walioshambulia hoteli ya kifahari ya Dusit D2 iliyoko kwenye majengo yaliyoko eneo la 14 Riverside jijini Nairobi, wananchi wameweza kumtambua gaidi mmoja ambaye waliishi naye mtaani kwa takribani miezi kumi.

Kwa mujibu wa majirani waliohojiwa na kituo cha runinga cha Citizen, gaidi huyo alipanga katika jumba moja la kifahari namba E 9 katika eneo la Muchatha, Ruaka jijini Nairobi. Imeeelezwa kuwa gaidi huyo aliyejitambulisha kwa majirani kama Ally Salim aliishi kwenye nyumba hiyo tangu Machi 21 mwaka jana.

Ingawa wengi walikataa kuonekana, jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Michael, alieleza kuwa kwa kipindi hicho chote hawakupata nafasi ya kumfahamu vizuri jirani yao huyo mpya kutokana na namna alivyokuwa akiishi.

“Tunaogopa… yeye alikuwa ni mtu wa kuingia tu na kutoka na hakuja kitambo, kwahiyo yeye ni mgeni kwetu,” Michael alisimulia.

Alipoulizwa alikuwa mtu wa aina gani katika kipindi hicho hasa alipokutana naye alijibu, “hawezi kukupita mkikutana naye tu lazima akusalimie.”

Alieleza kuwa kwakuwa mwenye nyumba hiyo haishi katika eneo hilo, wao huwapokea wapangaji wake kama majirani kwani wanajua watakuwa wameelewana na mwenye nyumba. Alieleza kuwa gaidi huyo alikuwa na mwanamke ambaye  muda wote alikuwa amejifunika kwa vazi la Burqa linalofunika mwili na sura na kuacha macho pekee.

Alieleza kuwa kwa makadirio ya kodi katika eneo hilo ambalo wanaishi watu wenye ukwasi, ni Ksh 50,000 (sawa na Sh 1,100,000 za Tanzania) kwa mwezi.

LIVE: Rais Magufuli akipokea hati za utambulisho wa Mabalozi

Citizen imezungumza na mmoja wa maafisa wa usalama ambaye ameeleza kuwa kwenye nyumba ambayo gaidi huyo alikuwa anaishi kulikuwa na shimo ambalo linaaminika kuwa ndimo walimokuwa wakificha silaha zao. Pia, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na vilipuzi kadhaa.

“Maafisa wa polisi wameniarifu kuwa hadi sasa hawajapata mhusika yeyote wa nyumba hii wakiwa wanaendelea na uchunguzi wao,” amesimulia ripota wa kituo hicho cha runinga.

Kwa mujibu wa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, magaidi wote wameuawa na hali ya utulivu imerejea nchini humo.

Watu 14 wamefariki kutokana na shamulio hilo.

Dar24 inatoa pole kwa Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa tukio hilo la kigaidi, na tunavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi na vyombo vya habari kwa jinsi walivyoshiriki katika kuwadhibiti magaidi.

Shahidi: Bilionea wa Unga ‘El Chapo’ alimhonga Rais wa Mexico
Magaidi walioshambulia hoteli Nairobi wauawa