Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Namungo FC Kindamba Namlia amesema kilichowakuta mjini Luanda, Angola walipokua wamekwenda kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya 32 bora Kombe la Shirikisho, kimewafunza jambo muhimu.

Kindamba amesema mazingira waliokutana nayo mjini Luanda, japo yalikua na maumivu kisaikolojia, yamewafunza mambo kadhaa ambayo wanaamini yatawasaidia katika ushiriki wao kimataifa.

Amesema endapo watafanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, watajihami kwa kuchukua tahadhari zote kabla ya kufanya safari ya kuelekea nchi yoyote ya Bara la Afrika, ili kujinusuru na mambo mabaya.

“Yote yaliyotokea yametupa funzo, hivyo tutajipanga vizuri zaidi kuelekea michezo yetu ijayo ya kimataifa,”

“Timu imerejea salama nchini bila wachezaji wake watatu na kiongozi mmoja ambao kimsingi kutokana na sheria za mamlaka ya afya wao wataendelea kubaki.”

“Wachezaji hao ambao ni Kikoti, Mgunya, Tangaru pamoja na Ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa klabu, Omary Kaaya watasalia kutokana na mamlaka zao kusema wana ugonjwa wa COVID-19, na wataruhusiwa kutoka Angola kama tu watapimwa na kugundulika hawana maambukizi.”

Msafara wa Namungo FC uilirejea nchini juzi usiku kutokea Angola ilipokwenda kwa ajili ya mchezo wa kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao Clube Desportivo 1º de Agosto ambao hapo awali ulipangwa kufanyika siku ya Jumapili.

Wakiwa nchini Angola, Namungo walikumbabna na matukio mengi ikiwemo wachezaji wao watatu ambao ni Lucas Kikoti, Hamis Mgunya, Fredi Tangaru na Ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa klabu, Omary Kaaya kutajwa na mamlaka ya afya za Angola kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona, huku viongozi wa Namungo wakitafsiri matukio hayo kama uhalifu wa kupanga uliofanywa kwa lengo la kuwadhoofisha.

Sakata hilo lilipelekea mchezo huo kufutwa na Shirikisho la soka Afrika (CAF), huku kamati maalum ikikaa kulijadili suala hilo, na kufikia muafaka wa michezo hiyo yote miwili kupigwa nchini Tanzania.

Juhudi za Namungo kurejea nyumbani na nyota wake wote ziligonga mwamba na kulazimika kuwaacha wale waliotajwa kuwa na Corona mpaka pale watakapopona.

Mexime azidi kuichimba Young Africans
Aliewapa 'PENATI' Mbeya City hatarini kufungiliwa