Mipango Namungo FC ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho Simba SC, Ibrahim Ajibu imeingia dosari, kufuatia mabingwa hao kuiweka kapuni ofa iliyowasilishwa mezani kwao.

Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu, amethibitisha klabu yake kuwasilisha ombi la usajili wa kiungo huyo, ili kuboresha kikosi chao kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao.

Amesema katika ripoti ya Kocha wao Mkuu, Thierry Hitimana, imependekeza majina ya nyota wawili kutoka Simba, Ajibu na Shiza Kichuya, ili kuboresha kikosi chake kuelekea michuano hiyo, jambo ambalo linaonekana kukwama kwa kiungo huyo aliyewahi kuitumikia Young Africans.

“Katika ripoti hiyo, Hitimana alitaja majina ya wachezaji akiwamo Ajibu na Shiza Kichuya, tumepeleka barua Simba kuomba nyota hao, wametujibu kuwa tutampata Kichuya, lakini si Ajibu kwa kuwa bado yupo kwenye mipango ya benchi lao la ufundi.

“Baada ya kumkosa Ajibu, sasa tunapambana kutafuta mchezaji mwingine, lakini (kocha) amewataka Iddi Mobby wa Polisi Tanzania, Abdulhalim Humud na Issa Rashid (‘Baba Ubaya’) kutoka Mtibwa Sugar,” amesema Zidadu.

Mbali na Ajibu pia amesema wamegonga mwamba katika mpango wa kumsajili Mobby na sasa wanasubiri maombi yao ya kuinasa huduma ya Humud na Baba Ubaya.

“Kuhusu wachezaji wetu, Blaise Bigirima tunatarajia kumalizana naye kwa kumwongeza mkataba mwingine baada ya hapo tutaendelea kuwaongezea wachezaji wengine akiwamo Reliants Lusajo pamoja na wale waliopendekezwa katika ripoti ya kocha,” amesema mwenyekiti huyo.

Namungo FC tayari imeshamsajili aliyekuwa kiungo wa Lipuli FC, Fredy Tangalo, kwa mkataba wa miaka miwili.

Tangalo, mchezaji pekee aliesajiliwa klabuni hapo tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa mwanzoni mwa mwezi huu Agosti.

Kiungo huyo amejiunga na klabu hiyo ya Ruangwa mkoani Lindi akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Lipuli FC.

Mbeya City watuma salamu Simba, Young Africans
Simba SC, Young Africans, Azam FC zavimbiana usajili 2020/21