Uongozi wa klabu ya Namungo FC umesema licha ya kufuzu kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao 2020/21, wanahitaji kutwaa ubingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) ili kuweka heshima.

Timu hiyo ya Namungo ishinde au isishinde mchezo wa Fainali utakaopigwa Agosti 02 mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, tayari ina nafasi kwa sababu Simba SC imeshakata tiketi yua Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushinda taji la Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Namungo FC Hassan Zidadu amesema wana mipango mikubwa ya kufanya vyema michuano ya kimataifa, hivyo baada ya kumaliza michuano ya ligi kuu wanasubiri ripoti ya kocha wao kuona uwezekano wa kufanya maboresho ya kikosi chao kujiandaa vizuri zaidi.

Amesema lengo ni kuona sio wanashiriki tu michuano hiyo mikubwa Afrika, bali wanafanya vizuri na kuandika historia nyingine mpya.

“Tunataka kuwa timu ya kwanza Lindi sio tu kushiriki michuano ya kimataifa, bali kuchukua taji la ASFC, kwa hiyo bado hatujaridhika tunajipanga kuhakikisha lengo letu linatimia,” amesema mwenyekiti wa Namungo FC Hassan Zidadu.

“Hatutaki kuwa kama timu nyingine zilizopita tunashiriki kisha tunafanya vibaya, tunataka kuwa na kikosi bora ambacho kitapambana, ni lazima tujipange kusajili wachezaji wenye uwezo,”amesema.

Amewaahidi mashabiki wa soka kuwa hawatawaangusha kama ilivyotokea kwa baadhi ya timu, bali watafanya kweli kwa kuonyesha umakini wa ushiriki wao na kufanya vizuri zaidi.

Namungo ilikata tiketi ya kucheza hatua ya Fainali baada ya kuitandika Sahare All Stars ya Tanga bao moja kwa sifuri mwishoni mwa juma lililopita, huku Simba wakiwafuata kwenye hatua hiyo kwa kuibanjua Young Africans mabao manne kwa moja.

Rais Magufuli amtaja mteule wake kijana kama mfano wa viongozi kuridhika, ana PhD
Simba SC kusaka heshima VPL