Timu ya Namunngo FC imekata tiketi ya kucheza Fainali Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC), baada ya kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Sahare All Stars.

Sahare All Stars waliokua nyumbani Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, walikatishiwa ndoto zao wa kusonga mbele kwenye michuano ya ASFC dakika ya 80, kufuatia bao lililofungwa na Edward Manyama.

Hata hivyo haikuwa rahidi kwa Namungo FC kupata bao hilo la ushindi kutokana na mchezo huo kukabiliwa na ushindani mkubwa kwa timu zote kusaka ushindi, ambapo dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika bila kufungana.

Namungo FC ilitinga Nusu Fainali kwa ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Alliance FC ya Mwanza, mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi juma lililopita.

Sahare All Stars ambayo ilikua timu pekee inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kutinga hatua ya nusu fainali ilishinda mbele ya Ndanda FC kwa mikwaju ya Penati nne kwa tatu baada ya dakika 90 kukamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Uwanja wa CCM Mkwakwani.

Kwa mantiki hiyo Namungo FC wanamsubiri mshindi wa mchezo wa kesho, Julai 12 kati ya Simba SC dhidi ya Young Africans, kwa kucheza hatua ya fainali mjini Sumbawanga mkoani Rukwa mwanzoni mwa mwezi ujao.

Kwa mara ya kwanza Trump avaa barakoa hadharani
Klopp: Jordan Henderson hadi 2020/21