Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Namungo FC, wameingia kambini kujiandaa na mchezo wa hatua ya kwanza dhidi ya El Hilal Obeid ya Sudan.

Namungo FC walitinga kwenye hatua hiyo, baada ya kuiondoa Al-Rabita ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao matatu kwa sifuri, huku mchezo wa mkondo wa pili ukifutwa na Shirikisho la soka Barani Afrika CAF.

Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemedi Morocco, amesema wameweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo dhidi ya El Hilal Obeid, ambao utachezwa Desemba 23, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini, Dar es Salaam, kabla ya mchezo wa pili kupigwa mjini Khatoum, Sudan mwanzoni mwa mwezi ujao.

Morocco amesema akiwa kambini visiwani zanaibzr atayafanyia kazi mapungufu aliyoyaona kwenye kikosi chake, kupitia michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara United Mara na kisha Azam FC, ambayo kwa pamoja waliambulia alama mbili kwa kuambulia matokeo ya sare.

“Awali tulikuwa na changamoto katika safu ya ushambuliaji, nimelifanyia kazi na naona mabadiliko kwa kutumia nafasi hizo vizuri, kuelekea michuano ya kimataifa tunahitaji kuwa makini kulingana na wapinzani wetu,” amesema Morocco.

Katika hatua nyingine kocha Morocco amethibitisha kuwafuatilia El Hilal Obeida kupitia video na hivyo anakiimarisha kikosi chake kwa ajili ya kuwakabili na hatimaye kupata matokeo mazuri.

Mfumo wa kielektroniki kupanga hoteli
Kortini kwa kosa la kutumia youtube bila kibali