Michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya iliyo katika hatua ya nusu fainali itaendelea tena hii leo kwa mchezo wa mkondo wa pili kati ya mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich dhidi ya Atletico Madrid kutoka nchini Hispania.

Atletico Madrid iliyoibuka na ushindi wa nyumbani wa bao 1-0 juma lilipita itakuwa na kibarua kigumu cha kukamilisha azma yake ya kutinga fainali kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu.

Bayern watakuwa na kibarua kigumu Zaidi cha kupindua jedwali la mabao kwa kuwa wanahitajika kufunga mabao dhidi ya ukuta mgumu wa Atletico ya kocha Diego Simeone aliyebobea katika soka la kutibua mipango na kubana wapinzani.

Frank Ribery yupo fiti kuelekea mchezo huo kama taarifa za kitabibu zinavyosema huku kocha wake Pep Guardiola akijivuania uwepo wake na imani yake ni kwamba atawasidia kupindua matokeo katika usiku wa Ulaya.

Manuel Nuer atakuwa na kazi ya kupangua mashuti ya kina Antoine Griezman na kuisadia timu yake kupata ushindi wa kuanzia mabao mawili ili kuwasukuma nje ya mashindano Atletico wanaosifika kwa soka nguvu.

Kama wengi wanavyofikiria ndiyo uhalisia ulivyo, bado mchezo huu upo wazi kwa maana unatoa fursa kwa yeyote kutinga hatua inayofuata licha ya Atletico kuwa mbele kwa bao hali inayozidi kuufanya mchezo wenyewe kuwa mgumu na usiotabirika.

Mbivu na mbichi zitabainika baada ya kipenga cha mwisho cha mwamuzi kupulizwa kuashiria mwisho wa mtanange.

Mtoto Mchanga atolewa hai chini ya Kifusi Kizito baada ya jengo la ghorofa 6 kuporomoka
Young Africans Hatarini Kupoteza Huduma Ya Kocha