Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye amefafanua namna ambavyo sheria inayovitaka vyombo vya habari kuwalipa wasanii mirabaha kutokana na kutumia kazi zao za sanaa itakavyotekelezwa kuanzia Januari Mosi.

Nape ameeleza kuwa vyombo vya habari vyote bila kujali ni vyombo vya kijamii au vya dini visivyotegemea kupata faida ya kifedha, vitatakiwa kugawana kipato chao na wasanii bila kujali ni kiasi kidogo kwa kiwango gani.

Alisema kuwa tayari serikali imeshapata mtambo wa kutambua nyimbo za msanii fulani zimepigwa mara ngapi katika kila kituo na kwamba wameipa kazi kampuni ya CMEA kukusanya taarifa hizo na kuziwasilisha COSOTA.

Alisema kuwa kila radio na TV italipa mrabaha kulingana na faida wanayoipata kutoka kwenye matangazo yao. Nape alisema viwango vya tozo ya mrabaha vitatofautiana kulingana na ukubwa wa chombo cha habari na faida kinayopata.

“Ukisema Chombo hakijiendeshi kwa faida maana yake wangekifunga. As long as chombo kipo, basi lazima kuna faida fulani wanaipata. Na kila chombo hakitalipa flat rate. Chombo kinachopata matangazo mengi kitalipa kiasi kikubwa zaidi cha fedha, na kinachopata tangazo moja kitalipa kwa mahesabu ya tangazo hilo,” Nape aliiambia SAUT FM Radio iliyoko jijini Mwanza.

Nape alitangaza kuanza kutumika kwa mfumo huu kuanzia Januari Mosi mwakani. Hata hivyo, baadhi ya wadau wakiwamo vyombo vya habari wameonekana kukosoa uamuzi huo kwa madai kuwa bado hawajashirikishwa vya kutosha katika kuingia kwenye mfumo huo.

Mfumo wa kuwalipa wasanii kwa kucheza kazi zao kwenye radio na TV unatumika katika nchi nyingi Afrika huku Afrika Kusini ikidaiwa kufanikiwa zaidi kutumia mfumo huu kutokana na jinsi ilivyojipanga.

Babu wa Loliondo Amshauri Magufuli Kuhusu Afya, atoa utabiri wa Muujiza Mpya
Umoja Wa Afrika Kutuma Wanajeshi 5000 Burundi