Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametolea ufafanuzi taarifa zilizosambaa kwenye mitandao kuwa alipiga marufuku vyombo vya habari kuripoti maandamano ya vyama vya upinzani hususan Chadema yanayodaiwa kuwa ya kichochezi.

Nape ameeleza kuwa hakuzuia vyombo vya habari kuripoti mikutano na maandamano ya upinzani kama ilivyoelezwa, bali amekataza vyombo hivyo kuripoti matamshi ya uchochezi yanayotolewa.

“Nilitoa tahadhari kuwa kama shughuli hizo zitakuwa na uchochezi wa aina yoyote ni marufuku kwa vyombo vya habari kuripoti. Kwa sababu vikiripoti vitakuwa ni sehemu ya huo uchochezi. Ukiripoti mtu anayezungumza uchochezi, maana yake unasaidia kusambaza huo uchochezi, na unakuwa sehemu ya huo uchochezi,” Nape aliuambia mtandao wa Millardayo.

Waziri huyo wa Habari alivitaka vyombo vya habari nchini kutumia busara na weledi wanaporipoti habari mbalimbali za kisiasa ili wasiingie katika hatari ya kukumbana na adhabu.

Akizungumzia adhabu inayoweza kuvikuta vyombo vya habari vitakavyoripoti matukio na kauli zenye uchochezi kuwa ni pamoja na kuvifuta.

“Adhabu nimewaambiwa ni kupewa onyo, kufungiwa kwa muda fulani, na adhabu ya juu zaidi ni kufuta kabisa katika orodha ya vyombo vya habari,” alisema.

Hivi karibuni, Waziri huyo alitangaza kulifungia gazeti la Mseto linalomilikiwa na kampuni ya Hali Halisi kwa sababu alizoeleza kuwa imeandika habari za uongo na za uchochezi.

Video Mpya: AY - El Chapo
Mkurugenzi Wa Halmashauri Ya Bunda Apokea Madawati 90 Ya Chadema Yaliyokuwa Yamekataliwa Na Madiwani Wa Ccm