Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo imeandikia barua klabu ya Yanga kuiagiza iwe imekwishafanya uchaguzi wake hadi kufika Aprili 15, mwaka huu.

Yanga imekwishapokea barua hiyo kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wakisistizwa hilo ni agizo la Waziri  wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye.

Pamoja na kwamba wapo kwenye maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kesho dhidi ya Al Ahly, lakini tayari Yanga wameanza kulifanyia kazi agizo la Serikali na wakati wowote wanaweza kutangaza uchaguzi.

Lakini kuna wasiwasi kama uchaguzi unaweza kuwa umefanyika hadi Aprili 15, kwa sababu muda waliopewa ni mfupi mno kukamilisha taratibu.

Yanga inapaswa kuutangaza japo kwa wiki moja uchaguzi, kugawa fomu kwa wagombea japo kwa wiki moja pia, na baada ya hapo ipatikane angalau wiki moja nyingine kwa ajili ya usaili, mapingamizi kabla ya kupiga kura kuchagua viongozi.

Yanga kwa sasa ipo chini ya uongozi ambao umekwishamaliza muda wake, chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji na Makamu, Clement Sanga.

Manji na Sanga waliingia madarakani Julai 15, mwaka 2012 katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu akiwemo Mwenyekiti Wakili Lloyd Nchunga na Makamu wake, Davis Mosha.

Walichaguliwa pamoja na Wajumbe Abdallah Bin Kleb, Moses Katabaro, Aaron Nyanda na Geroge Manyama ambao waliungana na Wajumbe waliobaki, akiwemo Salum Rupia na Mohammed Binda.

Hata hivyo, baada ya uongozi huo kumaliza muda wake mwaka 2014, Manji akaunda Kamati ya Muda, yeye na Sanga wakiendelea na nyadhifa zao.

Video Hii ya Simba aliyepambana na mafuriko Kenya yapata umaarufu
Wenje apigwa chini rasmi Mahakamani, Mabula ashinda kesi ya ubunge