Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape na Nnauye ameitaka jamii kuwatenga na kuwakataa wasanii wanaotumia sanaa kuwadhalilisha wanawake.

Nape aliyasema hayo jana Bungeni alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Mary Mwanjelwa (CCM) aliyetaka kupata ufafanuzi wa Serikali kuhusu kudhibiti udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wasanii nchini.

Waziri huyo aliwataka viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuungana kukemea na kuwakataa wasanii hao na kwamba kwa kufanya hivyo wataacha kufanya matendo hayo.

“Ikiwa jamii itayakataa matendo [mabaya] yanayofanywa na wasanii, wasanii hao wataacha kufanya haya matendo. Lakini ikiwa jamii inayashabikia na kuyapenda, wasanii hao wataona ndio fashion na wataendelea kuyafanya,” alisema Nape.

“Kila mtanzania akiona kuwa akidhalilishwa mwanamke, amedhalilishwa mzazi wake, amedhalilishwa ndugu yake, nadhani haya matendo yatakoma. Kwahiyo nadhani ni suala la jamii yetu kuwakataa na kuwatenga wale wanaofanya shughuli za kuwadhalilisha mama zetu,”  aliongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alieleza kuwa ili kuendelea kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya wasanii nchini, wasanii wakataobainika kufanya hivyo wataendelea kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwapiga faini ya malipo ya fedha.

Joto La Pambano La Leo, Masau Bwire Aamikia Uwanja Wa Uhuru
Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Latakiwa Kusimamia Ahadi ya milioni 50 za Rais Magufuli Alizoahidi kwa Kila Kijiji