Serikali imetoa siku saba kwa wamiliki wote wa vyombo vya habari wanaodaiwa na waandishi wa habari waliofariki katika ajali ya gari wilayani Busega kulipa madai yote waliyokuwa wakidai.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa agizo hilo wakati akiongoza shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa waandishi watano na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki dunia jana.

“Nimepewa salamu hapa kuwa miongoni mwa waliolala kwenye majeneza hapa mbele yangu wapo ambao hawajalipwa stahiki zao; natoa siku saba kwa waajiri wote wanaodaiwa kulipa stahiki zote za marehemu na kutoa taarifa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza,” ameagiza Nape.

Akionyesha msisitizo kuhusu agizo hilo, Waziri huyo aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari wanoadaiwa kutambua kwamba wizara yake ndiyo imeshikilia leseni zao.

“Yawezekana kuna hali ngumu ya kiuchumi, lakini nasema stahiki zote za marehemu hawa zilipwe ndani ya siku saba. Hayo ya hali ngumu tutayazungumza huko mbeleni kwa waandishi ambao wako hai ila kwa hawa marehemu lazima walipwe,” ameagiza Waziri Nape.

Awali, wawakilishi wa waandishi wa habari waliotoa salamu walimuomba waziri huyo kushughulikia changamoto ya waandishi kutolipwa stahiki zao huku wakifichua kuwa baadhi ya marehemu hawajalipwa kwa miaka miwili iliyopita.

Waandishi hao wa habari 5 walifariki katika ajari ya gari iliyotokea wilayani Busega mkoa wa Mwanza wakati wakielekea katika ziara ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza wilayani Ukerewe.

RC Singida atoa maagizo kwa kamati tendaji mradi wa korosho
Mwanahabari wa marekani apata umaarufu Kenya kutokana na giza.