Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye amejibu hoja za Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa waliosusia vikao vya Bunge vinavyojadili Mpango wa Maendeleo wa Mwaka wa Fedha 2016/17.

Jana, Wabunge wa Ukawa wakiongozwa na kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe, walitoka nje ya Bunge na kususia kikao cha Bunge wakidai kuwa hawatashiriki Mpango huo na kutoa mpango mbadala kwakuwa Serikali imekuwa ikivunja Katiba na Sheria za nchi pamoja na kuingilia madaraka ya Bunge.

Wabunge hao pia walieleza kupinga uamuzi wa Serikali kusitisha urushwaji wa Matangazo ya vikao vya Bunge Moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa na kuzuia vyombo vya habari kuripoti moja kwa moja mikutano ya Bunge.

Nape ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mtama amejibu hoja hizo akieleza kuwa Wabunge hao wameshindwa kumudu kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo wameshindwa kuja na Mpango mbadala.

“Tunachokiona hapa sisi pengine wenzetu kasi ya awamu ya Tano imewashinda ndio maana wameshindwa kupata mpango mbadala wa kuuweka hapa, badala yake wameanzisha vioja wanasema wao hawaweki kuleta mpango huo,” alisema Nape.

“Hizo hoja za kusema kwamba Katiba inavunjwa, taratibu zinakiukwa… lakini ziko namna za kushughulikia ukiukwaji wa Katiba na ukiukwaji wa taratibu. Cha msingi tu kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inawapa shinda na ndio maana wameshindwa kuja na mpango mbadala,” aliongeza.

Nape aliwataka Watanzania kuwapuuza wapinzani huku akiwashauri kurudi Bungeni kupitisha mpango ulioandaliwa na Serikali ikiwa wameshindwa kuja na mpango mbadala.

Waliochukua Mikopo kwa majina Ya Watumishi Hewa waonja rungu la Magufuli
Magufuli azungumzia kuhama kwa ‘Akina Lowassa’