Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amewataka Watanzania kujifunza kuwatia moyo Wanamichezo wanaposhiriki katika michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Wito huo ameutoa jana Jijini Dar es Salaam wakati wa Hafla ya kuwapongeza na kupokea bendera ya Taifa toka kwa Wanamichezo ambao walishiriki katika Mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika hivi karibuni mjini Rio, nchini Brazil.

Mhe. Nnauye alisema kwamba, Watanzania ni vizuri wakajifunza kusema maneno mazuri kwa wanamichezo pindi wanaporejea toka katika Mashindano mbalimbali ili kuwapa moyo wa kuendelea kufanya vizuri wanamichezo hao huku akisisitiza kuwa, ni vema ukosoaji ukaendana na ushauri mzuri wenye kujenga badala ya kulaumu.

Aliongeza kuwa, Wanahabari nchini wanapaswa kuandika mazuri yanayofanywa na wanamichezo kwani yana manufaa kwa Taifa badala ya kutafuta maneno yasiyo na tija ya kukosoa mara kwa mara kwani kuna wavunja moyo wanamichezo.

“Tukijifunza kuandika na kusema mabaya tu ya kuvunja moyo kwa wanamichezo wetu hii sio sawa sawa, tujifunze kuwatia moyo, na hii ni hatua ya kwanza na wito wangu kwa Watanzania wote”, alisema Mhe. Nnauye

Alisisitiza kwamba, Watanzania wanapaswa kujifunza kujivunia vitu vya kwao kwa njia hiyo itakuwa ikiongeza hamasa kwa wanamichezo katika kujituma kwa manufaa yao na ya Taifa.

Aidha, alisisitiza kuwepo na maandalizi ya mapema kwa Wanamichezo nchini ili waweze kufanya vizuri zaidi huku akishauri uwekezaji wa kutosha katika sekta hiyo na kuyataka Makampuni kuwa na tabia ya kuwatumia Wanamichezo nchini katika kutangaza utalii wa nchi.

Ametoa wito kwa Viongozi wazembe ambao watashindwa kufikia malengo mazuri katika tasnia hiyo ni bora wakaachia ngazi zao ili kuwapa nafasi watu wengine wenye uwezo kutekeleza kazi hiyo.

“Nadhani sasa tuanze kukabana kwenye Vyama, ukichaguliwa na kukawa na mashindano kama haya, ukashindwa kupeleka hata mchezaji mmoja, kazi yako ya kwanza nadhani ni kijiuzulu”, alisema Mhe. Nnauye.

Awali akitoa taarifa ya Wanamichezo walioshiriki katika Mashindano hayo, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Bw. Gulam Rashid alisema kwamba, Tanzania ilishiriki mashindano hayo ikiwa na Wanamichezo saba, walimu wa tatu wa michezO ya kuogelea, Judo na riadha ambapo kati yao wachezaji wa nne walipata nafasi ya upendeleo (Universality).

Alifafanua kuwa, wachezaji wa nne waliofanikiwa kupata nafasi ya upendeleo ni wale ambao walishiriki katika michezo mbalimbali katika kusaka viwango, lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufikia viwango vinavyowaruhusu wao kushiriki katika mashindano hayo, hivyo kulingana na Sera na itikadi za Olimpiki zilitaka kila nchi Duniani ambayo ni Mwanachama wa Mashindano hayo kutoa watu wake, hivyo walitoa nafasi hiyo kwa wale waliokosa kufikia viwango kuweza kushiriki.

“Nchi ambayo haikuwa na wachezaji waliofikia viwango vya Olimpiki walipewa nafasi ya upendeleo kwa wanamichezo kuweza kushiriki na kwa Tanzania tulikuwa na Waogeleaji wa tatu, mchezaji wa Judo na mchezaji wa kike wa mbio (Marathon) kwa hiyo, huo ndiyo upendeleo ambao wengi hawauelewi ni upendeleo upi”, alisema Bw. Gulam.

Aidha, katika hafla hiyo, mbali na kukabidhiwa Bendera ya Taifa toka kwa kikosi hicho cha Wanamichezo walioshiriki katika Olimpiki 2016 mjini Rio-Brazil, Mhe. Nnauye kwa niaba ya Makampuni ya TTCL na DSTV-Multi Choice aliwapatia zawadi mbalimbali washiriki hao zikiwemo fedha taslimu ambapo kwa nafasi ya kipekee Mwanariadha Alphonce Simbu ambaye aliibuka katika nafasi ya tano katika Mashindano hayo amepatiwa Mkataba wa mwaka mmoja wa kuwa Balozi wa DSTV ambapo kila mwezi atakuwa akilipwa kiasi cha Shilingi milioni moja pamoja na king’amuzi maalum, huku washiriki wengine wakipewa ving’amuzi na fedha.

Lipumba Aendelea Kung'ang'ania Uenyekiti Wake CUF
Msanii Kutoka Nigeria YCEE Atoa Msaada Kituo Cha Kulelea Watoto Wanaoishi Katika Mazingira Magumu Kigamboni Community Center