Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amedai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimevamiwa na watu aliowaita wasaka tonge ambao kazi yao ni kuvumisha tuhuma za uongo dhidi ya makada wa chama hicho.

Nape ametumia mtandao wa Twitter usiku wa kuamkia leo, kutoa ujumbe huo kufuatia taarifa zilizowekwa mtandaoni na mtu anayejiita ‘Sauti ya Kisonge’, aliyevalia mavazi ya chama hicho.

Katika tuhuma hizo, watu hao wamedai kuwa Nape, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe pamoja na vigogo wengine wa zamani wa chama hicho wanahusika na kuanzishwa kwa chama kipya kinachoitwa USAWA na kwamba hali hiyo ndiyo iliyomuibua Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally.

Kupitia ujumbe wake, Nape amedai watu hawa hawajui Imani na itikadi ya chama hicho tawala bali wanaamini matumbo yao, huku akisisitiza kuwa watu hao aliowaita waongo watatoka ndani ya chama lakini wenye chama akiwemo yeye wapo sana.

 

“Niliposoma upuuzi huu sasa NINA AMINI CCM imevamiwa na wasaka tonge wasiojua Imani wala Itikadi ya Chama! Hawana wanachoamini isipokuwa matumbo yao! Uongo huu ni kwa faida ya nani? Watatoka wao, wenye Chama tupo sana!”


Kauli hiyo ya Nape imekuja wakati ambapo bado kuna vuguvugu la Membe kuitwa katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM ili kujibu tuhuma za kutaka kuhujumu mchakato wa uchaguzi wa kumpitisha mgombea urais wa chama hicho mwaka 2020. Tuhuma zilizoanza kupeperushwa na Syprian Musiba.

Maseneta nchini Marekani wamshukia Mwanamfalme wa Saudia
Lugola awaomba wananchi kuwajengea polisi, ‘wahurumieni’