Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametengua uteuzi wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya kutokana na kutorishwa na kasi ya utendaji wake.

Waziri Nnauye alitengua uteuzi huo katika ziara yake aliyoifanya leo mapema katika ofisi za BMT kwa lengo la kuona miundo mbinu ya ofisi hizo na pamoja na  changamoto walizonazo.

Lihaya

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Henry Lihaya

Hata hivyo, alibaini kuwa baraza hilo limeendelea kudumaa kiutendaji huku mazingira ya ofisi zake yakiwa hayana mpangilio maalum wa kiofisi wenye taswira chanya ya uwepo wa ofisi hiyo kwenye eneo husika.

Hivyo, Waziri huyo alitangaza kumtimua Lihaya katika nafasi ya Utendaji Mkuu akiielezea hatua hiyo kama sehemu ya mkakati wa kusaidia kuongeza kasi ya utendaji katika Baraza hilo.

“Lakini pia tukusaidie kukubadilishia Mtendaji Mkuu. Tukupe mtu anayeweza kuongeza kasi, akaleta mawazo mapya hapa. Kwahiyo Mtendaji Mkuu aliyopo nitamuomba Katibu Mkuu amtafutie kazi nyingine ya kufanya wizarani,” alisema Nnauye.

Alimtaka Mwenyekiti wa Baraza hilo kuwasilisha mapendekezo ya mtu anayetaka kumteua ili ashike nafasi iliyoachwa wazi na Lihaya ili aweze kuyapitisha.

Kadhalika, Nape alimuahidi Mwenyekiti wa Baraza hilo kuwa Serikali itawasaidia kuwapatia watumishi wa kutosha na namna ya kutengeneza vyanzo vingine vya mapato ili liweze kujiendesha.

Henry Lihaya amefanya kazi katika Baraza hilo kuanzia mwaka 2009, lakini kasi yake ya utendaji wa miaka 7 umeonekana kuzorota.

 

 

 

Simba Yaendelea Kuneemeka Na Usajili Wa Kimataifa
Chama la Wana Lajinasibu Kurejesha Heshima Nyumbani