Vyama vya michezo nchini vimeshauriwa kujenga ofisi zao ndani ya uwanja wa Uhuru kuepukana na gharama za kukodi ofisi katika maeneo mengine.

Ushauri huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakati akipokea Uwanja wa Uhuru uliokuwa unafanyiwa  matengenezo na  kampuni ya CBG.

Mhe. Nape Moses Nnauye amesema kuwa mpaka sasa michoro kwa ajili ya majengo ndani ya Uwanja huo ipo tayari na vyama vya michezo vinakaribishwa kuanza kujenga ofisi zao.

“Kama kuna vyama vya michezo vyenye uwezo binafsi au kama wanaweza kupata ufadhili wa kuja kujenga ofisi zao humu michoro ipo tayari na eneo lipo tayari ata kesho waje wajenge ” alisema Mhe. Nape.

Mhe. Nape amesisitiza kuwa zoezi hili litaratibiwa na Serikali moja kwa moja na kutoa nafasi kwa vyama vyenye uwezo kujitokeza na kuchangamkia fursa hiyo ambapo  ramani,michoro na eneo lipo tayari kwa ajili ya zoezi hilo.

Aidha Serikali imewaalika wadau mbalimbali kuwekeza katika michezo kwa kujenga miundombinu itakayosaidia kukuza vipaji kwa wanamichezo mbalimbali na kusukuma gurudumu la  maendeleo ya sekta ya michezo nchini.

Kwa upande wake katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel amevishauri vyama vya michezo nchini kuchangamkia fursa iliyotolewa na Serikali ya kujenga ofisi za vyama vyao ndani ya Uwanja wa Uhuru na kushauri wadau wa michezo kuwekeza zaidi katika michezo hasa kwa vijana.

“ Wadau kimbilieni fursa ndio hii ya kuwekeza katika michezo pamoja na vyama vya michezo kujenga ofisi zao ndani ya Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya maendeleo yao na michezo nchini” alisema Prof Gabriel.

Sheikh Mkuu Wa Mkoa Wa Dar es salaam Awataka Vijana Kutokutumika Na Wanasiasa
Video: BAVICHA - Tumeamua kumsaidia Rais Magufuli, Waomba kupewa ulinzi Septemba 1