Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imefanikiwa kukodisha maeneo kwa ajili ya wafugaji kufuga mifugo yao hali iliyochangia kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku ikiahidi kuendelea kushirikiana na wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika ranchi hizo.

Akizungumza wakati wa kikao cha mwisho cha bodi ya wakurugenzi ya NARCO, mwenyekiti wa bodi hiyo Paul Kimiti amesema bodi hiyo ambayo imemaliza muda wake baada ya kukaa madarakani kwa miaka mitatu imeweza kwa kiasi kikubwa kusimamia na kuhakikisha wafugaji nchini ambao wana mifugo mingi wanapatiwa maeneo kwa mikataba katika ranchi hizo ili waweze kufuga mifugo yao na kukuza sekta ya mifugo nchini.

“Tumegawa maeneo ya ranchi takriban asilimia 75 na kubakiza asilimia 25 kwa kuwa wafugaji nchini wamekuwa na mifugo mingi na wanahitaji maeneo kwa ajili ya kufuga mifugo yao.” Amesema Bw. Kimiti

Aidha amesema katika kipindi cha miaka mitatu bodi ya wakurugenzi ya NARCO imeweza kuhakikisha maeneo ya ranchi za taifa yanawekewa mipaka ili kuzuia uvamizi wa maeneo hayo na kwamba zoezi hilo linaendelea katika maeneo mengine ambayo bado hayajawekewa alama hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NARCO Prof. Peter Msoffe amesema bodi ya wakurugenzi ya NARCO ambayo imemaliza muda wake imeweka misingi sahihi katika kufuatilia ukubwa wa maeneo ya ranchi, madeni na mashauri mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa yameiwezesha NARCO kupata mafanikio zaidi.

Kwa upande wao baadhi ya wakurugenzi wa bodi ambayo imemaliza muda wake wamesema kampuni hiyo imeweza kutatua kwa kiasi kikubwa migogoro baina ya wafugaji na watumiaje wengine wa ardhi kwa kuamua kukodisha vitalu kwenye ranchi za NARCO ili wafugaji waweze kufuga mifugo yao.

Wameongeza kuwa NARCO imekuwa ikifuga mifugo bora ambapo wananchi wanakaribishwa kwenda kununua mifugo hiyo ikiwemo ng’ombe na mbuzi ili kuwa na aina bora ya mifugo inayozalishwa katika ranchi hizo.

Pia wamewaalika wawekezaji kuwekeza katika ranchi za NARCO kwa ajili ya kulima malisho, kujenga majosho na miundombinu mbalimbali ili mifugo inayozalishwa katika ranchi hizo kuongezewa thamani.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Paul Kimiti akifafanua jambo kwa wakurugenzi wa bodi hiyo iliyokaa madarakani kwa miaka mitatu namna ilivyoweza kukodisha maeneo kwa ajili ya wafugaji kufuga mifugo yao hali iliyochangia kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu ya NARCO jijini Dodoma.
Wakurugenzi wa bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) wakiongozwa na mwenyekiti wa bodi hiyo Bw. Paul Kimiti wakiwa kwenye kikao cha mwisho cha bodi ambayo imekaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu. Kikao hicho kimefanyika katika makao makuu ya NARCO jijini Dodoma.

Miradi 41 kuchunguzwa na TAKUKURU
Habari Picha: kilele mbio za mwenge