Jashua Nassari, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameshangaa uamuzi wa Spika Job Ndugai kumfutia ubunge wake.

Jana, Spika Ndugai alitangaza uamuzi wa kumvua ubunge Nassari na kumuandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumueleza kuwa jimbo hilo liko wazi na achukue hatua stahiki za kuitisha uchaguzi.

Akizungumzia uamuzi huo, Nassari amekiri kutohudhuria vikao vitatu vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini amedai kuwa alimuandikia barua Spika wa Bunge kumueleza kuwa yuko nje ya nchi akimuuguza mkewe.

“Huu mkutano uliopita [wa Januari 29,2019 hadi Februari 9] nilikuwa nje ya nchi namuuguza mke wangu, alikuwa na matatizo ya uzazi na nilimjulisha Spika kupitia barua niliyoituma kwa barua pepe,” Mwananchi wanamkariri Nassari.

Kwa mujibu wa Mwananchi, Nassari alisema kuwa anashangaa uamuzi huo kwani hata kabla ya kuandika barua alizungumza na msaidizi wa Spika Ndugai ambaye alimshauri kuandika barua hiyo.

Nassari amekuwa mbunge wa kwanza kuchukuliwa hatua hiyo kutokana na sababu hizo, ambapo Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa uamuzi huo umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1)(c), ambapo ibara hiyo inaeleza kuwa ”Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake cha ubunge ikiwa ataacha kuhudhuria vikao vya mikutano ya bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.”

Korea Kaskazini waeleza kifuatacho baada ya Trump na Kim kushindwana
Naibu waziri Mabula agawa vifaa vya kujilinda ngozi Karagwe