Saa chache baada ya kuachiwa huru kutokana na amri ya Rais John Magufuli, Rapa Nay wa Mitego amesema kuwa atayafanyia kazi maoni ya Rais kuhusu kuboresha wimbo wake kwa namna ya pekee.

Rapa huyo alitiwa nguvuni wikendi iliyopita kwa tuhuma za kusambaza wimbo wake wa ‘Wapo’ ambao Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) liliweka wazi kuwa haufai na una lugha za matusi, lakini mambo yalibadilika baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kueleza kuwa amezungumza na Rais Magufuli na amesema anaupenda wimbo huo na kwamba ameagiza aachiwe huru na aufanyie maboresho kwa kuongeza mambo mengine bila kupunguza alichokiimba.

Akizungumzia suala hilo, Nay wa Mitego amesema kuwa ataufanyia marekebisho wimbo huo lakini atahakikisha havuki mipaka.

“Ninalifanyia kazi, mheshimiwa amesema anaupenda wimbo wangu na anausikiliza, yeye mwenyewe amewekwa kwenye huu wimbo ni jambo ambalo hawezi kupuuzia na hiki kinachoendelea labda amefurahishwa, hivyo nitaifanyia kazi kwa kuongeza mengi makubwa na kwa mapana zaidi bila kuvuka mipaka,” Nay wa Mitego anakaririwa.

Msanii huyo aliwataka wananchi na vyombo vya habari kuendelea kuzungumza ukweli na kutoa maoni yao lakini wazivuke mipaka.

‘Wapo’ haukuwa wimbo wa kwanza kumuweka matatani Nay wa Mitego kwani baadhi ya nyimbo zake kama ‘Pale Kati Patamu’ na ‘Shika Adabu Yako’ ziliwahi kufungiwa na Basata na kupewa onyo kali.

Mzimu Wa Lionel Messi Waizima Argentina
Sudan Kusini, Comoro Kucheza AFCON 2019