Na Allawi Kaboyo – Bukoba.

Benki ya Taifa ya Biashara NBC tawi la Bukoba imetoa msaada wa Saruji tani nne katika kusaidia ujenzi wa  vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Igabilo kufuatia shule hiyo kukumbwa na uhaba wa madarasa.

Akiongea kabla ya kukabidhi msaada huo, katika viwanja vya shule ya msingi Igabilo iliyopo Halmashauri ya wilaya Bukoba, Meneja wa Benki hiyo  tawi la Bukoba, Mathias Mhangilwa, amesema kuwa msaada  huo ni shukrani kwa wananchi ambao wamekuwa wateja wao, hivyo wamewiwa kurudisha kwa jamii kile wanachokipata kama faida.

“Msaada huu ni shukrani kwa jamii yetu tunayoihudumia maana tumekuwa tukifanya hivi mara kwa mara na kwa maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji ya eneo husika, hapa katika shule hii upo uhaba mkubwa wa madarasa hivyo tumeona  tuchangie ili kusaidia katika ujenzi wa madarasa mapya,” amesema Mhangilwa.

Mhangilwa ameeleza kuwa baada ya serikali  ya awamu ya tano kuanza  kutoa elimu bila malipo, kumekuwepo na ongezeko la wanafunzi ambalo linapelekea kuwepo kwa upungufu wa madarasa hali iliyowapelekea kuchangia katika ujenzi huo.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Bukoba Babylus Mashauri, ameishukuru benki hiyo kwa msaada huo ambao utawawezesha kujenga vyumba viwili vya madarasa ili kuweza kupunguza msongamano wa wananfunzi kwenye vyumba vya madarasa.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi shule hiyo ina wanafunzi 789 huku mahitaji ya vyumba vya madarasa kwa mujibu wa maelekezo ya  wizara ya elimu ni vyumba 14, ambapo vyumba vilivyopo ni 9 na mapungufu ni vyumba 5 hali inayopelekea mrundikano mkubwa madarasani.

M-Lipa kutumia KwikPay kurahisisha huduma za malipo kwa wafanyabiashara
Rais Mwinyi awaapisha Mawaziri, awaagiza kuanza na hili