Fukuto lililojitokeza ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi baada ya Katibu Mkuu pamoja na mwenyekiti msaidizi wa chama hicho kutangaza kutoridhishwa na mwenendo wa mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi kupitia Ukawa, limepelekea kuwepo taarifa za tishio la kumuangamiza mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

Taarifa za kuwepo kwa njama za kutaka kumuangamiza Mbatia zilitolewa jana na mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la NCCR-Mageuzi ambaye pia ni mkuu wa idara ya Sheria, Haki za Binadamu na Katiba, Mohamed Tibanyendera.

Alieleza kuwa idara ya usalama ya chama hicho imepata taarifa za kiintelijensia kuhusu kuwepo njama za kumdhuru mwenyekiti wa chama hicho katika mkutano wa hadhara wa kampeni.

“Chama kimepokea taarifa kutoka idara ya usalama kuwa kuna watu wameandaliwa kuleta machafuko. Watavaa sare katika kampeni zinazoendelea na watavamia na kupiga viongozi, mlengwa mkuu ni Mbatia,” alisema Tibanyendera na kueleza kuwa chama hicho kimeziamini taarifa hizo kwa namna zilivyowasilishwa.

Alieleza kuwa Mbatia alishauriwa kufikisha taarifa za tishio hilo kwa jeshi la polisi na alifanya hivyo kwa kuwasilisha maelezo ya kuwepo tishio hilo katika makao makuu ya jeshi la polisi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na mwandishi wa gazeti la Mtanzania, msemaji mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alipotaulizwa aliwataka wana habari kumuamini James Mbatia bila kutoa ufafanuzi wa moja kwa moja kama tayari jeshi hilo limeshapata taarifa hizo kutoka kwa Mbatia.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi anadaiwa kutopokea simu tangu taarifa hizo ziliporipotiwa.

 

Nikki Wa Pili: Davido Alivujisha Collabo Na Joh Makini
Magufuli Kufikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma Za Wizi