Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba Jumatano wiki hii alitumia mtandao wa Jamii Forums kutoa ufafanuzi na utetezi wake kuhusu sakata la kupotea kiutata kwa Benard Saanane ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Uamuzi wa Waziri huyo kutumia mtandao huo kujibu tuhuma hizo umevuta hisia za watumiaji wa mtandao huo ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Polisi kumkamata na kumfungulia mashtaka mmiliki wa mtandao huo, Maxence Melo.

Melo alishtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo kuendesha mtandao huo bila kusajiliwa pamoja na kuzuia upelelezi wa polisi kwa kuficha taarifa za watumiaji wake kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao ya Mwaka 2015

Waziri Nchemba ambaye alijiunga na mtandao huo tangu mwaka 2012, aliamua kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na mtu anayetumia jina la ‘technically’ aliyeandika maelezo yanayohoji kama waziri huyo hapaswi kuhusishwa na kupotea kwa Saanane.

Akijibu tuhuma hizo, Nchemba alieleza kuwa Saanane alikuwa rafiki yake ambaye anafahamika hata katika familia yake na kwamba walikuwa wakiwasiliana hata katika wiki ambayo alipotea baadae.

“Ben is my personal friend (Sio katika Siasa) tunakutana na kushirikiana mambo kila mara mpaka ya familia, namfahamu na anaifahamu familia yangu mpaka watoto wangu wanamfahamu. Nilimsaidia kura za maoni ndani ya chama chake, nimewasiliana naye mfululizo mpaka wiki hiyo hiyo. Unamwongelea rafiki yangu na ndugu yangu wa ndani, na sasa nafuatilia kama serikali na kama rafiki,” aliandika.

Waziri Nchemba alimtaka ‘technically’ kuacha kutoa tuhuma asizokuwa na ushahidi nazo hata chembe katika kipindi hiki ambacho familia ya Saanane iko gizani isijue aliko.

“Tafadhali, tuna mambo ya kisera tunaweza kupigana madongo, lakini hapa tunaongelea maisha ya mtu, an innocent young brother. Usikusanye vitu vya kuungaunga na kuleta katika jambo kubwa ambalo bado lina giza na wengine ni ndugu yao wa damu na wengine ni close friend,” aliandika Nchemba.

Alimtaka mtoa mada huyo kutoandika vitu kwa hisia zake tu na kumtaka aungane na watanzania wengine kumuombea Saanane awe salama hadi sasa.

Saanane alidaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha

Polisi waelezea jinsi walivyomhoji Lissu
Kanisa la EAGT lachangia shil. mil. 10 maafa kagera