Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewaasa Watanzania kuishi kwa upendo na ushirikiano ili kuweza kudumisha amani na kufichua maovu katika jamii.

Ameyasema hayo mkoani Morogoro aliposhiriki mazishi ya Sheikh Mkuu wa mkoa huo, Abdallah Mkang’ambe ambapo amesema kuwa marehemu alikuwa akiwaunganisha watu na kukemea uovu wowote unaotokea katika jamii na kutaka Tanzania iwe nchi ya amani.

Amesema kuwa kwenye jamii ya aina fulani inapotokea mtu amefanya kosa basi haitakiwa jamii nzima kuchafuliwa au kunyooshewa kidole kwani kosa linakuwa limetendwa na mtu mmoja.

“Inapotokea muislamu mmoja amefanya kosa haimaanishi kwamba kosa hilo litakuwa la dini ya kiislam bali linapaswa kuchukuliwa kama mtu mmoja hivyo hivyo kwa wakristo na hata makabila,”amesema Nchemba

Aidha, kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe steven Kebwe amesema kuwa mkoa wake umepata pigo kubwa la kuondokewa na mtu muhimu ambaye alisaidia kumaliza mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyodumu kwa kipindi kirefu.

Hata hivyo, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi amesema kuwa marehemu Sheikh Mkang’ambe alikua ni mmoja wa viongozi vijana wa mikoa aliokuwa anawategemea sana katika kujenga nguzo katika BAKATWA.

 

 

Video: Prof. Kabudi ampongeza JPM kwa kuunda kamati ya uchunguzi
Halmashauri zatakiwa kuongeza kasi ukusanyaji mapato