Mshambuliaji wa Young Africans Ditram Nchimbi amesema katika mambo ambayo hawezi kuyasahau tangu aliposajiliwa na mabingwa hao wa kihistoria, ni kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa jumla ya mabao matatu kwa sifuri.

Nchimbi amesema matokeo ya mchezo huo yalimvuruga sana hasa ikizingatiwa ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa nyota wengi wapya waliosajiliwa mwezi Januari akiwemo yeye mwenyewe.

Lakini pia, ulikuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Luc Eymael ambaye alitua kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria mwezi huo huo.

“Kwa kweli ule mchezo ulituumiza sana wachezaji pamoja na kocha (Eymael), ulikuwa ndio mchezo wetu wa kwanza. Wachezaji wengi wageni tulianza kuonekana pale baada ya kukosa michuano ya kombe la Mapinduzi,” amesema

“Hata hivyo wakati mwingine inabidi kukubali, kuna wakati mpira unakuwa na matokeo ya kikatili sana, ” aliongeza.

Nchimbi amekuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Young Afrcans akiwa amefunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao.

Jumla amefunga mabao 5 kwenye ligi, matatu akiwa ameifunga Yanga wakati akiitumikia Polisi Tanzania.

Ni miongoni mwa wachezaji ambao mashabiki wa Young Africans wameweka matumaini makubwa kwao kuelekea msimu ujao

Uwezo wake wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji pamoja na winga, unampa nafasi zaidi ya kuendelea kutamba kwenye kikosi cha Eymael.

Elias Maguri: Usiogope Kuanza Upya
Bigirimana aipa masharti Young Africans