Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amewahakikishia wanafunzi wanaoendelea na masomo wakinufaika na mkopo kupitia Bodi ya Mkopo wa Elimu ya Juu kuwa hakuna atakayefutiwa mkopo.

Profesa Ndalichako aliyasema hayo jana Bungeni mjini Dodoma katika kikao cha Bunge la 11 kinachoendelea.

“Serikali haijafuta mkopo kwa mwanafunzi yoyote ambaye anaendelea na masomo yake,” alisema Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa kuchelewa kwa mkopo kumetokana na vyuo husika kuchelewa kuwasilisha matokeo ya wanafunzi wanaoendelea kwani hutumika kuwatambua wanafunzi wanaokidhi kigezo cha ufaulu.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa Elimu aliiagiza Bodi ya Mikopo kuhakikisha inawasilisha fedha za mikopo kwa vyuo vyote leo kwani Serikali ilishatoa fedha hizo tangu Oktoba 15 mwaka huu.

Wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini wamekuwa wakilalamika kwa kucheleweshewa mikopo yao huku baadhi ya waliokuwa wakiendelea na masomo wakiondolewa kwenye orodha ya wanaopata mkopo kwa madai kuwa wamekosa sifa.

Kutokana na hali hiyo, kundi kubwa la wanafunzi, baadhi wakiwa na wazazi wao wasiojiweza walifika katika ofisi za Bodi ya Mikopo jijini Dar es Salaam kulalamikia hatua hiyo.

Bodi hiyo ilitoa muda kwa wanafunzi waliokumbwa na panga hilo kuandika barua za kukata rufaa na kujaza upya taarifa zao, agizo ambalo limekutana na changamoto ya baadhi ya viongozi wa Serikali za wanafunzi za vyuo vikuu kulipinga na kuwataka wanafunzi hao kutojaza tena taarifa hizo kwani tayari walishajaza awali na kupewa mikopo.

Takribani wanafunzi 3,000 waliokuwa wamepata mikopo waliondolewa kwenye orodha ya wanufaika.

Asasi za Kiraia zaanzisha harakati kudai katiba mpya, zawatenga wanasiasa
Video: Magufuli azungumzia mafanikio ya serikali yake