Imefahamika kuwa, aliyekua kiungo mshambuliaji wa Young Africans Mrisho Khalfan Ngasa ametangazwa kujiunga na Ndanda FC itakayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2020/21.

Ngassa alikuwa sehemu ya wachezaji walioachwa na Young Africans baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jamboa mbalo lilizua gumzo kwa wadau wengi wa soka nchini.

Ndanda FC wamethibitisha kumsajili kiungo huyo, baada ya kuwasilisha orodha ya wachezaji waliowasajili kwa msimu mpya wa Ligi Daraja la kwanza.

Afisa Habari wa Ndanda FC ya Mtwara, Idrisa Bandari, amesema wamekamilisha usajili wao kwa ajili ya msimu mpya na mmoja wa nyota waliofanikiwa kunasa saini yake ni Ngasa.

“Tumekamilisha usajili wa Ngasa, tunapokwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, tunahitaji wachezaji wakomavu na wenye uwezo ambao watatusaidia kupanda tena Ligi Kuu,” alisema Bandari.

Aliwataja wachezaji wengine waliowasajili ni pamoja na Paul Ngalema na William Lucian ‘Gallas’, Henry Joseph Shindika, Stamil Mbonde na Jerry Tegete.

Katika hatua nyingine imeelezwa kuwa uongozi wa Ndanda FC ulikua na mpango wa kuwasajili wachezaji walioachwa na Young Africans Juma Abdul na Kelvin Yondani, lakini dakika za mwisho mambon yalikwenda tofauti.

Wakati huo huo, beki wa kulia Hassan Kessy aliyekua akiitumikia klabu ya Nkana FC ya Zambia, ametua kwa wakata miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar.

Ukurasa wa Instagram wa Mtibwa Sugar ulithibitisha taarifa za kusajiliwa kwa beki huyo ambaye aliwahi kutamba na klabu kongwe nchini Simba na Young Africans, pamoja na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar, Ibrahim Hamad Hilika kutoka Zimamoto kwa kumpa mkataba wa miaka miwili.

Nana: Sina mahusiano na yeyote, zaidi ya....
Sven: Hakuna mchezo rahisi mbele yetu