Wakati mashabiki wa Ndanda FC waliopo mjini Mtwara wakilalamika timu yao kuja kucheza mechi yao na Young Africans jijini Dar es Salaam, viongozi wa timu hiyo wamewaambia kwamba watulie kwao wao wamefuata pesa na si vinginevyo.

Mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona Jumamosi lakini sasa itachezwa Uwanja wa Taifa baada ya Young Africans kuomba ichezwe hapa kwani Jumapili wanatakiwa kusafiri kwenda Angola kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Esperanca.

Ndanda tayari wapo kambini Kibaha tangu jana Jumanne na baada ya mechi hiyo wataelekea Mbeya kwa ajili ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Mbeya City.

Msemaji wa Ndanda Idrisa Bandali alisema: ”Watu hawaelewi lengo letu ni lipi, Young Africans hawajatupa pesa yoyote na sisi tumekubali tukilenga zaidi kupata pesa nyingi za kwenye mapato ya mlango maana kila kitu tunasimamia sisi kama wenyeji wa mchezo.

”Ni kweli mashabiki wetu watakosa burudani ila wanapaswa kutuelewa tu, tunahitaji pesa na kipindi hiki tutazipata kwenye mechi hiyo pekee iliyobaki pesa ambayo itatusaidia kufanya mambo mengine kwani tunaamini mashabiki wengi watakuja Taifa kuishangilia timu yao ya Young Africans, ila tumeangalia na uzalendo kwa Young Africans wanaokwenda kuiwakilisha nchi,” alisema.

Young Africans ndiyo mabingwa wa VPL na Jumamosi watakabidhiwa kombe lao wakati Ndanda wao wamejihakikishia kubaki kwenye ligi msimu ujao.

Hamisi Kilomoni: Viongozi Wa Simba Wamejaa Ubinafsi
Mpinzani wa Museveni ajiapisha kuwa Rais, Kilichomkuta…