Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hii leo Novemba 17, 2022 imeshindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba Mkoani Kagera, kutokana na hali mbaya ya hewa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Anga (TCAA), Hamza Johari amesema ni kweli amepata taarifa hizo na kwamba Rubani alifuta safario ya Bukoba na hivyo kutua salama jijini Mwanza.

“Ni kweli nimepata taarifa za Ndege ya Air Tanzania imeshindwa kutua kutokana na hali mbaya ya hewa, kulikuwa na ukungu, Mvua, Radi na Giza uwanja ukawa hauonekani,” amesema Hamza.

Usafiri wa Shirika la Ndege la Tanzania, ATCL.

Mara baada ya kushindwa kutua katika uwanja huo, Rubani wa ndege hiyo alilazimika kurejea Mwanza na kutua salama baada ya uwepo wa ukungu, mvua, radi na giza na kufanya uwanja huo kutoonekana.

Kufuatia tukio hilo, Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira ameandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa “Still shaken (bado natikiswa), lakini Mungu ni mwema.”

Andiko la Mbunge huyo liliengelea kusema, “Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba, safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua, nampongeza rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar, Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba.”

Ndege ya Precision Air iliyopata ajali Mjini Bukoba – Kagera.

Novemba 6, 2022 Ndege ya Precision Air iliyokuwa na watu 43 ilianguka katika Ziwa Victoria na kuua watu 19, baada ya kushindwa kutua katika uwanja wa Bukoba kutokana na hali mbaya ya hewa.

Kufuatia ajali hiyo, Baraza la Mawaziri liliagiza kuwa uchunguzi unaofanywa na mamlaka husika uhusishe wataalamu wa ndani na nje ya nchi, ili kubaini chanzo na kushauri hatua stahiki.

Masauni ateta na Wajumbe vyombo vya Usalama
Rais Samia apewa Tuzo ya Heshima amani na utulivu