Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amegawa kompyuta 25 kwa shule za sekondari za Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe zenye thamani ya shilingi milioni 48 kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kujifunzia na waalimu kufundishia, kuongeza uelewa na kupata maarifa kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)

Amekabidhi kompyuta hizo kwa Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Ludewa ili ziweze kutumika kwenye shule mbalimbali zilizopo Wilayani humo.

“Nimeleta kompyuta 25 ili zigawiwe kwenye shule mbalimbali ili watoto wajifunze kutumia TEHAMA pamoja na walimu waliopewa mafunzo ya TEHAMA na taasisi yetu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), amesema Nditiye. Kompyuta hizo zimetolewa na UCSAF ambayo inahusika na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara,”amesema Nditiye

Aidha, ameongeza kuwa Wilaya ya Ludewa inafahamika katika kipindi cha miaka ya nyuma kwa kuwa moja ya Wilaya saba nchini ambapo wanafunzi wake wana kipaji cha akili ukilinganisha na Wilaya nyingine zilizopo nchini.

Kwa upande wake Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere kuwa, kuwe na kituo kimoja cha kutunga mitihani Ludewa ili walimu watunge mtihani wa aina moja na waweze kumaliza kufundisha masomo ya kiada na ziada kama walivyopanga.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Andrea Tsere amemueleza Naibu waziri Nditiye kuwa wataweka intaneti kwenye kompyuta hizo ili walimu na wanafunzi waweze kupata notisi, huku akiahidi kuwa kompyuta hizo zitatumika kuinua kiwango cha elimu na zimefika muda muafaka.

 

Majaliwa akabidhi Jenereta kituo cha afya Mkowe
DCB yatakiwa kuwajengea uwezo wateja wake

Comments

comments